Alhamisi, 14 Aprili 2016

HOTUBA YA MH. UMMY MWALIMU, KATIKA UZINDUZI WA BARAZA LA LA WATAALAM WA AFYA YA MAZINGIRA NCHINI AWAMU YA TATU!


HOTUBA YA MHE. UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWENYE UZINDUZI WA BARAZA LA USAJILI WA WATAALAM WA AFYA YA MAZINGIRA NCHINI TAREHE 14/04/2016.

·        Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
·        Mganga Mkuu wa Serikali,
·        Mkurugenzi wa Idara ya Kinga,
·        Mwenyekiti wa Baraza la Usajili wa Wataalam wa Afya ya Mazingira Nchini,
·        Msajili Baraza la Usajili wa Watalaam wa Afya ya Mazingira Nchini,
·        Wasajili wa Mabaraza wa Kada za Afya,
·        Wajumbe wa Baraza la Usajili Wataalam wa Afya ya Mazingira,
·        Wataalam wa Afya ya Mazingira Nchini,
·        Wanahabari,
·        Wageni Waalikwa,
·        Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema. Pili, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote  kwa kufika kwenu kushuhudia kuzinduliwa kwa Baraza hili la Wataalam wa Afya ya Mazingira nchini awamu ya tatu. Aidha, nawapongeza sana wajumbe wote wa Baraza lililopita kwa kuendeleza kazi za kuliimarisha Baraza la Afya Mazingira. Leo hii tunapokea wajumbe wapya kuendeleza yale yaliyoanzishwa katika awamu ya kwanza na ya pili na sasa ni awamu ya tatu ya utekelezaji. Aidha, ningependa kuwashukuru wote ambao mmeacha shughuli zenu na kukubali kuitikia wito wa kuja kushiriki pamoja nasi katika tukio hili muhimu na la kipekee katika historia ya kada ya afya ya mazingira nchini. Nawashukuruni sana.

Ndugu Mwenyekiti,
Afya ya Mazingira ni eneo muhimu na nyeti, ambalo utekelezaji wake unajikita zaidi katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza katika jamii yetu. Serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli imeona umuhimu wa suala hili hususan pale ambapo sherehe za Uhuru zilipobadilishwa na kuadhimishwa nchi nzima kwa kufanya usafi wa mazingira ili kuonyesha kuwa maendeleo ya taifa lolote yanategemea afya za wananchi wake. Kauli mbiu Mtu ni Afya na Kinga ni Bora Kuliko Tiba zimekuwa zikitumika sana kwa nguvu zamani wakati wa uhuru. Kaulimbiu hizi bado zina umuhimu katika maisha yetu ya hivi sasa hivyo, tunapaswa kuikumbusha jamii yetu kuwa kila mwananchi anapaswa kuwekeza kwenye usafi wa mazingira kwa kuanza  na kudumishaji usafi binafsi, usafi wa nyumba yake ya kuishi, usafi katika eneo lake la kazi, usafi katika vyombo vya usafiri, usafi katika sehemu za biashara, usafi katika nyumba za kulala wageni, usafi katika sehemu zinazouza vyakula, usafi na usalama wa vyakula na maji, usafi katika viwanda, migodi, mashamba, taasisi na nk. Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa kila sehemu inahitaji kuwekwa katika hali ya usafi na endelevu ili kudumisha kanuni za afya mazingira.

Ndugu Wananchi,
Katika ya miaka hivi karibuni, Serikali imefanya maboresho katika sekta ya afya nchini ambayo yanalenga katika kuimarisha na kudumisha huduma bora za afya ya msingi kote nchini. Miongoni mwa masuala muhimu ni kuweka msingi na taratibu za kuhakikisha watoa huduma za afya wanazingatia sheria, kanuni, miiko na maadili ili waweze kutoa huduma kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu. Pamoja na mambo mengine Serikali imetunga Sheria ya Kusimamia na Kudhibiti Utendaji wa  Wataalamu wa Afya ya Mazingira  ya mwaka 2007, na kutengeneza Kanuni za Ujumla za Sheria zinajulikana kwa jina la kiingereza “The Environmental Health Practitioners (General) Regulations 2011”. Kanuni ya 3, 4 na 5  zinazungumzia suala la Usajili, kuorodheshwa na kuandikishwa kwa Wataalam wa Afya ya Mazingira Nchini. Aidha Kanuni ya 12 ya Kanuni za Ujumla za Usajili inasisitiza kusajiliwa kwa wataalam wote wenye taaluma ya Afya Mazingira kote nchini. 



Ndugu Wananchi,
Napenda kutoa msisitizo juu ya suala hili kwa kuzitaja huduma za afya ya mazingira  zinazostahili kusajiliwa na Baraza la Afya Mazingira kama ifuatavyo; Huduma za kuzoa, kuhifadhi, kusafirisha na kutupa taka, kunyonya, kusafisha, kusafirisha na  kumwaga maji taka, huduma za Kuuza vyakula (mahoteli, migahawa ya aina zote, maoko ya mikate, maduka yauzayo nyama, maduka ya vyakula, viwanda vya vyakula, Kuuza maji, Kuuza vyakula kwenye sherehe,  uuzaji juisi mbalimbali na shughuli za kukoboa na kusaga nafaka). Huduma za viwanda vinavyozalisha kemikali, vumbi, mionzi. Huduma zinazozalisha taka hatari zitokanazo na huduma za kidaktari (health care wastes). Huduma za kusafisha na ufagizi wa ofisi, mitaa, mifereji ya maji machafu, ukusanyaji na uteketezaji  takataka (incinerators services). Huduma za uangalizi wa dampo na uchambuzi wa taka rejea (recycling). Huduma ya upuliziaji dawa za Viuatilifu kwenye maghala, hospitali, mashamba, majumbani, maofisi na kwenye vyombo vya usafiri. Huduma za Vyoo vya Jumuiya, vyoo vya muda (mobile and temporary toilets). Huduma za nyumba za kulala wageni, maeneo ya kuogea (swimming pool), kinyozi na  ‘saloons’ za  aina zote. Huduma zitokanazo na Biashara zinazozalisha machukizo ‘offensive trades’ (kuchoma mifupa, kukaanga samaki, kukausha majongoo).  Huduma za utengenezaji majeneza na maziko ya wafu. Haya yote yamebainishwa katika Kanuni ya Ujumla ya Usajili (GN 388 ya tarehe 25 Nov. 2011).
Ndugu Mwenyekiti,
Taaluma ya Afya ya Mazingira ni muhimili muhimu katika kupambana na magonjwa ya mlipuko. Shirika la Afya Ulimwenguni ambapo Tanzania ni miongoni mwa mwanachama, lilitengeneza Kanuni za Afya za Kimataifa (The International Health Regulations) kwa mujibu wa Kanuni hizi wataalamu wa Afya Mazingira ndio wasimamizi wakuu wa Kanuni hizi na wana wajibu wa kuhakikisha kuwa wageni wote wanaoingia nchini kupitia katika mipaka yetu wanakaguliwa kwa kusudi la kuzuia magonjwa yanayoripotiwa Kimataifa.  Nchi nyingi zinazoendelea hivi leo zinakabiliwa na changamoto ya wataalamu wa afya mazingira kukosa tekinolojia ya kisasa na endelevu, vitendea kazi duni, mazingira duni yasiyoridhisha kiafya, hali mbaya ya uchumi, soko la ajira, uzembe na uzururaji, Rushwa, ushindani wa kitaaluma, mabadiliko ya tabianchi (kuongezeka kwa joto duniani), matumizi ya kemikali na viuatilifu yasiyozingatia misingi ya afya mazingira. 
Katika sekta ya Afya, kuna changamoto nyingi zikiwemo za ongezeko la magonjwa ya milipuko yatokanayo na uchafuzi wa mazingira, hususan ugonjwa hatari wa kipindupindu. Aidha, Afya Mazingira ni suala mtambuka ambalo linahusisha  wadau wengi katika kulitekeleza. Ni muhimu katika utekelezaji wa majukumu yake, Baraza lishirikishe kwa karibu wadau mbalimbali kutoka sekta mbalimbali  ili kutoa matokeo chanya yenye tija na ubora wa hali ya juu kwa taifa letu. Ni matumaini yangu kuwa tutafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kupunguza ama kuondoa changamoto nyingi zinazotukabili kwa kusudi la kuzuia maambukizi ya magonjwa.

Ndugu Mwenyekiti,
Kwa muda mrefu, kumekuwepo  matukio ya ukiukwaji wa maadili katika utoaji wa huduma za afya ya mazingira nchini, ambapo matatizo ya kitaalam hutolewa maamuzi bila ya kuzingatia taratibu na misingi ya taaluma. Hili ndilo lilipelekea kuanzishwa kwa Baraza la Usajili wa Wataalam wa Afya ya Mazingira nchini kama chombo pekee cha kusimamia na kudhibiti utendaji wa Wataalamu wa  Afya Mazingira nchini. Utendaji wa Baraza litakalozinduliwa leo unatakiwa kuwa wa kasi zaidi, katika maamuzi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora. Aidha, nawaasa Wataalamu wa Mazingira nchini mbadilike na kufanya kazi kwa weledi, umahiri, bidii na kwa kuzingatia mongozo ya maadili na nidhamu ya kazi ili kuinua hali za Afya za wananchi.

Ndugu Wananchi,
Ni matarajio ya Serikali kuwa kwa kutumia  Baraza hili kama chombo cha Taaluma ya Afya Mazingira, yafuatayo yatainufaisha jamii yote ya watanzania;
·  Huduma ya afya ya jamii  hapa nchini itatolewa kwa viwango vinavyotakiwa na hivyo kuboresha maisha ya wananchi Baraza litasimamia na kudhibiti utoaji wa huduma ya afya ya mazingira kwa misingi ya haki.
·        Wataalam wa kada hii watajiendeleza  ili kuinua kiwango cha taaluma ya Afya Mazingira.
·   Kuendelea kutengeza kanuni, viwango vya utoaji huduma na kuweka taratibu sahihi za kiutendaji zinazoendana na wakati.
·        Kumaliza tatizo la ugonjwa wa kipindupindu nchini na kupunguza kasi ya magonjwa ya kuambukiza.

Ndugu Mwenyekiti,
Sheria imeweka bayana na kuainisha majukumu na mamlaka ya Baraza kama ifuatavyo;
·     Kuweka bayana majukumu ya makundi ya wataalamu wote wanaostahili kusajiliwa na hivyo kutoa huduma ya afya ya mazingira hapa nchini chini ya Sheria hii.
·        Kuweka bayana adhabu zitakazotolewa kwa wataalamu watakaokiuka kanuni, taratibu na maadili vya kitaalamu ya wataalamu wa fani hii kwa mujibu wa Sheria.
·        Kusajili wataalamu wa afya ya mazingira kulingana na viwango vya utaalamu wao pamoja na taasisi zinazotoa huduma za Afya Mazingira.
·        Kuweka vipengele mbalimbali vya kisheria ambavyo vitasimamia utekelezaji wa kazi za Baraza n.k
·        Kuainisha vyanzo vya mapato mbalimbali ya baraza kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zote za Baraza.

Ndugu Mwenyekiti,
Katika kuhakikisha kuwa Baraza la kusajili wataalamu wa afya ya mazingira linafanya kazi yake ipasavyo, sheria imebainisha  muhula wa utendaji kazi Baraza teule, kuwa ni miaka mitatu kuanzia tarehe ya uteuzi kipindi hiki sio kirefu. Lakini tunayo matarajio makubwa sana kwenu. Nawaomba kufanya kazi kwa bidii ili kuwa kielelezo, tumieni muda wenu vizuri katika kufanya maamuzi yenye tija kwa wakati ili kuendeleza taaluma bila kuruhusu uzembe kazini ili ifikapo Mwaka 2018 kazi zitakazokuwa zimefanyika iwe kielelezo bora na mfano wa kuigwa na Baraza litakalopokea kijiti.

Baada ya kusema hayo machache nitoe rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu hawa wa Afya ya mazingira nchini kwa vile majukumu yao yanategemea sana ushirikiano wenu. Aidha nawaagiza wataalamu wa afya ya mazingira nchini kufanyakazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya Nidhamu na Maadili Kitaaluma. Nitumie fursa tena hii kuliagiza Baraza litekeleze majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya Sheria ili kudumisha utawala bora.

Baada ya kusema hayo napenda sasa nitamke kuwa Baraza la Usajili wa Wataalamu wa Afya Mazingira Awamu ya Tatu leo tarehe 14 Aprili, 2016 limezinduliwa Rasmi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni