Alhamisi, 7 Aprili 2016

MAGONJWA 10 YA KURITHI AMBAYO NI MUHIMU KUPIMA AU KUYAJUA NA MPENZI WAKO KABLA YA KUZAA MTOTO.


Magonjwa ya kurithi ni yapi?
Haya ni magonjwa ambayo yapo kwenye koo za watu fulani na hurithiwa kutoka kizazi mpaka kizazi lakini pia magonjwa haya huweza kutoka kwa mwanamke na mwanaume ambao kwa macho ni wazima kabisa na kuzaa watoto wenye matatizo ya kiafya.

Kwenye jamii zetu za kiafrika ni jambo la kawaida sana kuzaa tu bila kupima kujua kama kuna hatari ya kuzaa mtoto mwenye matatizo makubwa ya kiafya kutokana na vimelea vya kurithi yaani DNA ambazo wazazi husika wamezibeba, mimba nyingi zimekua zikisingiziwa kwamba hazikupangwa na wakati kila mtu anajua mwisho wa ngono zembe bila njia yeyote ya uzazi wa mpango ni mimba.
Hii ni tofauti na nchi zilizoendelea ambapo wazazi hupima vipimo hivi kabla ya kuamua kuzaa na hata ikigundulika mtoto anayekuja atakua na matatizo mimba hiyo hutolewa ili kuepusha maumivu ambayo mtoto huyo angeyapata kama angezaliwa na maumivu ya kisaikolojia na kiuchumi ambayo wazazi wanaozaa watoto kama hawa wanayapata, hii ni kwasababu ya kulazwa mara kwa mara kwa mtoto husika na kushindwa kufanya kazi maisha yake yote.

Hivyo nchi zilizoendelea watoto wanaozaliwa na magonjwa ya kurithi wametokomezwa kwa kiwango kikubwa sana tofauti na afrika ambapo watoto hawa ni wengi sana na kila siku wanazidi kuzaliwa, wakati wangeweza kuzuilika kama sisi wahusika na serikali ingechukua hatua kukomesha hili kwa kuingiza vifaa vya kitaalamu ya kuyagundua magonjwa haya muhimu.
Ni kweli vipimo vingi havipatikani hasa maeneo ya vijijini na hata mijini lakini kuna watu ambao wako kwenye nafasi kubwa ya kuzuia na kupunguza idadi ya watoto hawa wanazaliwa kila siku, hasa watu wanaoishi mijini na wenye uwezo kifedha lakini hata wewe ambaye huwezi kupata vipimo hivi hebu jaribu kwenda ukweni kwa mumeo au mkeo unaweza ukaona ugonjwa wa kurithi ambao sio wa kawaida huko na kufanya maamuzi vizuri au unaweza ukamuuliza mumeo au mkeo ili awe muwazi kabla ya kufunga ndoa kwani magonjwa mengine yanaonekana kwa macho tu.
Magonjwa haya ni kama yafuatayo


1.Sickle cell disease;{siko seli] huu ni ugonjwa wa kurithi ambao mtoto hurithi kutoka kwa baba na mama ambapo wazazi wawili ambao wanakua hawana dalili yeyote hubeba ugonjwa huu kwenye damu zao yaani carrier na wanakua na uwezekano wa 25% ya kumzaa mtoto huyu ambae ataugua na kua na dalili zote za ugonjwa huu. Ugonjwa huu ni hatari sana. Mwaka 2013 ugonjwa huu uliua watu laki mmoja na elfu sabini na sita duniani kote wengi wakitokea Africa hasa chini ya jangwa la sahara. Watoto hawa huanza na dalili za kuvimba vidole wakiwa na umri wa miezi mitatu, kuvimba vichwa, kua na miguu na mikono mirefu na miembamba, kulalamika maumivu makali, kuishiwa damu sana  na kadhalika ukubwani. Kama wapenzi wakipimwa wakakutwa wote wameubeba ugonjwa huu kwenye damu zao yaani carriers ni vizuri wakaairisha ndoa hiyo kwani watakaribisha matatizo makubwa kwenye maisha yao. Kama unataka kujua umebeba ugonjwa huu ukienda hospitali kubwa za rufaa wana uwezo wa kuwapima na kujua. Ugonjwa huu pia unaweza kupimwa kwa kuchukua maji kwenye tumbo la mama kabla hajazaliwa hivyo kuamua kuendelea na mimba au kuitoa. Japokua kutoa ni kosa kisheria nchini Tanzania. Watoto hawa huishi kwa mateso makali na 50% watakufa kabla ya miaka 40 kwa nchini kwetu Tanzania hakuna data kamili za watu hawa lakini wasichana wengi wenye ugonjwa huu hufa wanapoanza kuziona siku zao kwani damu hupungua zaidi na viungo vingi kushindwa kazi.

2.Haemolytic diseases of the new born;  kuna aina kuu nne za group za damu yaani A, B, AB, na O ambazo group hizo mtu anaweza kua positive au negative mfano mtu mwingine anaweza kua A positive na mwingine akawa  A negative au B positive na mwingine B negative.Sasa swala ni kwamba watu wa negative wakioana hakuana shida au watu wa positive wakioana hakuna shida LAKINI mwanaume wa positive akioa mwanamke wa negative mtoto wa kwanza atazaliwa vizuri lakini ataacha vitu vinaitwa antibodies ambavyo kazi yake itakua ni kuharibu mimba zote zitakazofuata kutoka kwa mwanaume huyu. Kipimo hichi ni rahisi sana na kinapatikanakaribia hospitali zote Tanzania na hata kama mmeshaoana tayari na mna tatizo hili kuna dawa maalumu inaitwa RHoGAM mama mjamzito anachomwa wiki ya 28 mpaka 32 kuzuia vifo hivyo.
 3.Albinism{Ualbino]: huu ni ugonjwa wa kurithi ambao motto huzaliwa bila vimelea vya melanin au kua na uchache wa vimelea hivyo ambavyo humfanya mtu apate rangi ya ngozi yake. Mara nyingi wazazi wote wawili wa mtoto huyu hubeba ugonjwa huu kwenye miili yao bila kua na dalili yeyote na wao kumzaa mtoto ambaye ni albino lakini pia kuna aina za ualbino ambazo mzazi mmoja anaweza kusababisha albino kuzaliwa bila mama kua na vimelea vya ualibino.Mtoto huyu huzaliwa akiwa na matatizo ya kutoona vizuri na makengeza, ngozi na nywele nyeupe sana. Kua albino sio ugonjwa lakini watu hawa hua kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kansa ya ngozi. Sio rahisi kupima kujua kama mtu anabeba vimelea vya ualbino kwenye mwili wake lakini inawezekana kupima mtoto aliyeko tumboni na kugundua kama nia albino au sio kwa nchi zilizoendelea au unaweza kumjua mwenzako kwa kuona albino kadhaa kwenye ukoo wao.
 4.Magonjwa ya akili: katika jamii kuna watu hua wanafanya vitu ambavyo sio vya kawaida mpaka unajiuliza huyu mtu amechanganyikiwa au vipi..yaani ni mtu wa fujo, hajifunzi kwa makosa ya nyuma, unasikia mtu kamuua mzazi wake,anavunja sheria mara kwa mara, kunywa pombe sana, anakasirishwa na vitu vidogo sana au maisha yake ya mahusiano yanakua ni ya ugomvi kila siku yaani kwa kifupi anakua tofauti na wengine. Dalili hizi sio za kupuuzia kuna uwezekano mkubwa sana wa kuzaa watoto wa aina hii ambao huanza kusumbua tangu wakiwa shule ya msingi na kupata matatizo makubwa ukubwani. Shida hizi hazihitaji vipimo ni wewe kutoa maamuzi mapema kabla hamjaamua kuzaa naye kwani mambo hayo yanarithiwa na mimi nimeshashuhudia familia nzima ya watu waliokua hawana akili nzuri yaani walikua wehu kabisa.
5.Magonjwa ya kansa; ugonjwa wa kansa haurithiwi lakini kuna baadhi ya koo zina vimelea{genes] ambazo baadae husababisha kansa. Ni vizuri kujua vyanzo vya vifo vya ndugu wa mwenza wako kabla ya kuamua kuzaa naye kwani ugonjwa huu unaweza kua ni mbaya zaidi kuliko magonjwa yote ya kurithi. Kuna familia naifahamu nyumba ilifungwa kwani watu wote waliuawa na kansa yaani mume na watoto wote waliozaliwa, dada na kaka wote wa mume isipokua mke tu aliyekua ameolewa pale.
6.Ugonjwa wa kisukari; ugonjwa huu yaani diabetes mellitus type 2 unawapata sana wagonjwa watu wengia ambao kwao kuna ugonjwa huu. Yaani kama baba yako na mama yako wana kisukari uwezekano wa wewe kupata kisukari ni asilimia hamsini. Maana yangu ni kwamba ukioa au ukiolewa na mtu ambao kwao kuna wagonjwa wa kisukari ujue kuna uwezekano wa mtoto wenu mmoja kuugua ugonjwa huo miaka ya baadae. Hivyo hua tunashauri kama wazazi wako wana kisukari kuepuka kua mnene kwani utakikaribisha mapema.
7.Ugonjwa wa asthma au pumu; ugonjwa huu ambao hushambulia mfumo wa upumuaji hufuata sana ukoo fulani wa watu japokua pumu zipo za aina mbili ile ya kurithiwa na ile ambayo sio ya kurithiwa hivyo kama ukoo unaoenda kuoa au kuolewa una wagonjwa wawili au watatu wa asthma kuna uwezekano mkubwa sana wa kumzaa mtoto mwenye pumu baadae, ugonjwa ambao huua haraka kama usipopata ufuatiliaji wa kutosha
8.Ugonjwa wa kifafa; japokua ugonjwa hu huweza kusababishwa na magonjwa mengine kama homa ya uti wa mgongo, ulaji wa nyama ya nguruwe na kadhalika ugonjwa huu umeonekana kufuata koo Fulani za watu yaani kama unaenda kuoa kwenye ukoo ambao unafahamu kuna wagonjwa wa kifafa uwezekano wa kuzaa watoto wenye kifafa upo hivyo ni vema kuingia unajua.
 9.Umbilikimo: huu ni ugonjwa wa kurithi ambao watu wanazaliwa sana kitaalamu unaitwa achondroplasia, wazazi wa watoto hawa ambao hua na mikino na miguu mifupi sana huweza kua kawaida kabisa lakini kutokana na kurithi vimelea vya ugonjwa huu hujikuta wanamzaa mtoto huyu na mtoto huyu baada ya muda Fulani akioa anazaa mtoto wa hivi hivi kwani mzazi mmoja tu huweza kusababisha hali hii.
 10.Magonjwa ya upofu; kuna koo ambazo watoto huzaliwa na vimelea vya hali ambayo husababisha upofu baadae au ikasababisha upofu hata kabla ya mtoto kufikisha miaka mitano. Mtoto huzaliwa na mtoto wa jicho kitaalamu kama congenital cataract ambayo huziba jicho taratibu na baadae mtu hataona kabisa na unaweza ukakuta ukoo una vipofu wengi na chanzo husika hakifahamiki.
Mwisho; haya ni baadhi ya magonjwa ambayo labda yameathiri watu wengi kwenye jamii zetu lakini yapo mengine mengi ambayo siwezi kuyataja na  makala hii haijaandikwa kuwatenga au kuwasema vibaya watu wenye matatizo haya kwamba wasioe au wasiolewe lakini ni kujaribu kuongea ukweli na kuepusha watu wenye tatizo moja kuzaa mtoto kwani ni kujiongezea matatizo tu kama nilivyosema hapo mwanzoni na kuleta viumbe ambavyo vinakuja duniani kuteseka sana. 

Ni bora waendelee kuzaliwa carriers yaani wanaobeba vimelea bila kuugua kuliko kuendelea kuwazaa wagonjwa.hivyo kama wewe unajua kwenu kuna shida fulani ni bora kuzaa na mtu ambaye kwao hamna shida kabisa kwani ukizaa na mtu mwenye matatizo kwao pia ni hatari zaidi na kama ukiamua kukaidi na  kuzaa hivyohivyo uzae unajua kwamba haya magonjwa yapo. niwape pole ambao tayari ni wagonjwa wa hali hizi na wale wenye ndugu wenye hali hizi.dunia inatambua maumivu yenu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni