Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo AFYA. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo AFYA. Onyesha machapisho yote

Jumamosi, 9 Julai 2016

Nguvu ya MAZIWA MTINDI kwa Wanawake na Wazee!


Maziwa ya mtindi hunywewa na hata kuwa mboga na chakula kwa watu wengi, lakini sasa kwa wanawake ni muhimu sana kunywa kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa wa fangasi.

Utafiti uliofanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umeeleza kuwa asilimia 70 hadi 90 ya wanawake nchini wanashambuliwa na aina mbalimbali za fangasi.

Wameeleza kuwa fangasi hizo zinatokana na sababu mbalimbali ambazo wanawake wanakumbana nazo katika maisha ya kila siku, ikiwemo ujauzito, matumizi ya kondomu kwa muda mrefu, kuchangia tendo la ndoa na mwanamume zaidi ya mmoja, nguo, maji, matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari na mazingira.

Utafiti huo umebaini sababu zinazochangia wanawake wengi kushambuliwa na vijidudu vya fangasi ikiwemo wanawake wenyewe kushindwa kujihifadhi vizuri. Aliongeza kuwa katika utafiti huo, walibaini pia kuwa wanawake wamekuwa wakishambuliwa na aina zaidi ya nne za fangasi.

Sababu nyingine alisema ni kutodhibiti matumizi ya sukari, ambapo fangasi huelemea kuta za seli na kuzalisha vimeng’ enya ambavyo hufyonza virutubisho na kuingia katika damu.

Fangasi baadaye huanza kujipenyeza kwenye damu, mapafu, moyo na hatimaye kushambulia figo ambapo huleta magonjwa nyemelezi na njia pekee ya kutibu ni kutumia mtindi mara kwa mara na kutumia dawa ambazo pia zinahitaji ushauri kwa daktari.

Utafiti huu ni muhimu kwa wanawake wote kuchukua hatua katika kupambana na fangasi ambao wakianza huwezi kujua kama wana maradhi kiasi hicho, lakini kila mmoja ahakikishe anatumia mtindi ambao ni chakula na dawa.

kila mwanamke ajikinge na kujitibu, ikiwa ni pamoja na kuona wataalamu wa afya kila unapoona dalili zozote za kuwa na fangasi. Lakini pia kuzingatia usafi wakati wote na namna ya kujihifadhi kama inavyoonekana kwenye utafiti huo, lakini kubwa zaidi ni kuhamasishana kunywa mtindi kwa ajili ya tiba hiyo.

FAIDA NYINGINE YA MAZIWA MTINDI :

Mtindi unaorodheshwa kuwa miongoni mwa vyakula bora kutokana na kuwa na virutubisho vingi vya aina mbalimbali ambavyo vina faida nyingi katika mwili wa binadamu.

Vikitajwa kwa uchache virutubisho hivyo, imethibitika kuwa mtindi ni chanzo kizuri cha ‘Calcium’, ‘Phosphorus’, ‘Riboflavin (vitamin B2), ‘Iodine’, ‘vitamin B12’, ‘Pantothenic acid (vitamin B5) ‘Zinc’, ‘Potassium’ na ‘Molybdenum’. Mbali ya virutubisho hivyo, ndani ya mtindi kuna ‘bakteria hai’ ambao ni muhimu kiafya katika mwili.

HUREFUSHA MAISHA:


Utafiti unaonesha kuwa unywaji wa mtindi mara kwa mara, hasa katika kundi la wazee, uwezo wa mwili wa kupambana na magonjwa mbalimbali umeonesha kuongezeka na kufanya mfumo wa kinga ya mwili kuwa imara zaidi.

Katika utafiti mmoja, walichaguliwa wazee 162 ambao walipewa utaratibu wa kunywa mtindi na maziwa zaidi ya mara 3 kwa wiki na kufuatiliwa maendeleo yao kwa muda wa miaka mitano. Baadaye utafiti huo ulionesha kuwa idadi ya vifo vya wazee hao ilipungua kwa asilimia 38 ukilinganisha na kundi la wazee wasiotumia au waliotumia mtindi kiasi kidogo sana.

KINGA KWA KINA MAMA:
Aidha, mtindi umeonesha kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa kinga dhidi ya maradhi ya kuambukiza ukeni (vaginal infections). 

Katika utafiti mmoja uliohusisha wanawake wenye magonjwa ya kuambukiza sehemu za siri, baada ya kutumia mtindi kiasi cha paketi moja kila siku kwa muda wa miezi sita, maambukizi waliyokuwanayo wanawake hao kabla yalitoweka.

KINGA YA MWILI:
Utafiti uliofanywa kwa wanyama, wakiwemo panya na kuchapishwa kwenye jarida moja la masuala ya virutubisho nchini Marekani (Journal Of Nutrition), umeonesha kuwa unywaji wa mtindi kila siku, huamsha na kuupa nguvu mfumo wa kinga ya mwili kupambana na magonjwa kadhaa ya maambukizi, ikiwemo saratani ya utumbo.

MUHIMU KUZINGATIA:
Jambo muhimu la kuzingatia ni unywaji wa mtindi halisi uliotengenezwa kutokana na maziwa halisi ya ng’ombe, siyo mtindi uliotengenezwa kutokana na maziwa ya unga. Siri kubwa iliyomo kwenye mtindi ni ule uchachu unaotokana na ‘bakteria hai’ wanaopatikana baada ya maziwa kuganda na kuchachuka.

Jumamosi, 7 Mei 2016

Serikali kwa kushirikiana na Taasisi zisizo za kiserikali nchini zaleta matumaini makubwa kwa watoto wenye matatizo ya Moyo!

DSC_3056
Mwenyekiti wa Taasisi ya Dhi Nureyn, Sheikh Said Ahmed Abri  akitoa hotuba  yake kwa wageni waalikwa (Hawapo pichani) wakati wa hafla hiyo.


Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imepongeza juhudi za Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Kiislam ya hapa nchini ya Dhi Nureyn Islamic Foundation kwa juhudi zake za kuunganisha nguvu na taasisi zingine za nje  katika kuokoa  maisha ya watoto wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo.
Akizungumza wakati wa hafla maalum ya kufunga kambi ya Moyo Muhimbili, Jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla amebainisha kuwa, Serikali inatambua juhudi za taasisi binafsi katika kusaidiana nazo hivyo kwa hatua hiyo, suala la magonjwa ya moyo ambayo awali yalikuwa yakitibiwa nje kwa sasa yatashughulikiwa hapa hapa nchini.
“Tunaishukuru taasisi ya Dhi Nureyn na taasisi zote kwa kushirikiana na taasisi ya JKCI, kwani zimeweza kusaidia kuokoa maisha ya watanzania ikiwemo kuokoa vifo ambavyo vingetokea kwa watoto wenye matatizo ya moyo.
Zoezi hili limeweza kuvuka lengo la asilimia 70. Kwa wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu hayo ya moyo.  Tunaamini mwaka huu tukaongeza malengo,  na tayari wameweza kufanya operesheni takribani 200. Hii ni misheni ya pili na kwa maana hiyo wameweza kuvuka malengo ya asilimia 70 yale tuliyowapa.” Alieleza Dk. Kigwangalla.
Kigwangalla amesema, awali kabla ya utaratibu  wa JKCI, wagonjwa 250 walikuwa wanapelekwa nje kufanyiwa operesheni hizo za magonjwa ya moyo. Lakini kwa mwaka huu hata miezi sita bado haijafika, Wagonjwa zaidi ya 200 wameshafanyiwa hapa hapa nchi operesheni hizo. Kwa hatua hiyo wameweza kuvuka lengo la asilimia 70 na wanataka wafikie angalau wagonjwa 400 hadi 500 kwa mwaka” alimalizia Dkr. Kigwangalla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya Dhi Nureyn, Sheikh Said Ahmed Abri  alieleza kuwa, taasisi hiyo imekuwa kiungo kuzitafuta taasisi zingine za nje ya nchi na kuleta wataalam hao bingwa wa magonjwa ya moyo hapa nchini.
Miongoni mwa taasisi hizo  zilziofanikisha kambi hiyo ya Moyo hapa nchini ni pamoja na Taasisi ya  Muntada Aid ya Uingereza, Timu ya Madaktai kutoka Saud Arabia, Taasisi ya RAF kutoka Qatar, Taasisi ya Dhi Nureyn (Tanzania) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (Tanzania). Zoezi hilo la kambi ya magonjwa ya moyo ni la pili kufanyika hapa nchini  likiwemo la kwanza la mwezi Mei mwaka jana (2015) na kufanikiwa kuwatibu watoto 66 wa Kitanzania ambao walipangiwa kwenda kutibiwa nje ya nchi na kufanya kuokoa mabilioni ya shilingi ya Serikali kwa ajili ya gharama za matibabu hayo.
“Tunaishukuru sana taasisi ya Muntada Aid, kwa kujali, kuthamini na kujitolea kufanya kazi hii iliyookoa maisha ya Watoto wengi na kuwaondoshea maumivu watoto na wazazi wao na kuwapa matumaini mapya ya maisha. 
Sheikh Said Ahmed Abri katika hotuba yake ametoa shukrani kwa Taasisi ya Jakaya Kikwete  na Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla pamoja na washirika wetu wote wakiwemo Taasisi ya Al Akhlaaq na wanahabari na wote kwa ujumla pamoja na mdaktari. 
Aidha, madaktari hao pamoja na taasisi zote zilizofanikisha zoezi hilo, zilitunukiwa vyeti na tunzo maalum kwa ajili ya shukrani.
DSC_2870

DSC_3112
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akipiga picha ya pamoja na Madaktari bingwa wa Moyo . Mwenye kanzu nyeupe  ni  Mwenyekiti wa Taasisi ya Dhi Nureyn Islamic Foundation, Sheikh Said Ahmed Abri, akifuatiwa na  Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya Moyo, Profesa Joom Joom  na mwingine ni daktari wa magonjwa ya Moyo aliyeambatana na timu hiyo ya madaktari hapa nchini
DSC_3133
Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya Moyo, Profesa Joom Joom akielezea jambo kwa waandishi wa habari (Hawapo pichani) namna walivyoweza kufanikisha Operesheni zilizofanyika hapa nchini hasa kwa watoto waliokuwa na matatizo ya Ugonjwa wa Moyo. Operesheni hiyo maalum ilifanyika kuazia Aprili mwaka huu na kumalizika mwezi huu wa Mei. Hafla hiyo imefanyika jana Mei 6.2016 Jijini Dar es Salaam. 
DSC_2873
Baadhi ya Madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete wakifuatilia hafla hiyo
DSC_2880
Prof. Jameel Alata ambaye ni kiongozi wa Madaktari Mwelekezi wa Magonjwa ya Watoto  akitoa shukrani zake kwa namna walivyoweza kufanikisha kambi hiyo ya Moyo hapa nchini.
DSC_2908
Mwenyekiti wa Taasisi ya Dhi Nureyn, Sheikh Said Ahmed Abri  akimkabidhi tuzo  Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi  katika kuthamini taasisi hiyo.
DSC_2923
Baadhi ya Madaktari waliokabidhiw vyeti vya shukrani:
DSC_3035
Mwenyekiti wa Taasisi ya Dhi Nureyn, Sheikh Said Ahmed Abri  akiabidhi tuzo kwa mgeni rasmi, Mh. Dk. Kigwangalla kwa namna Serikali inavyothamini mchango wa taasisi binafisi hapa nchini.
                                                         (Picha zote na Andrew Chale,)

Jumatatu, 25 Aprili 2016

TAMKO LA WAZIRI WA AFYA MHE. UMMY MWALIMU KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MALARIA DUNIANI APRIL 25.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO


TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU (MB) - WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MALARIA DUNIANI
TAREHE 25 APRILI, 2016

·        Viongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya  Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
·        Kamati za usimamizi wa huduma za afya Mkoa na Wilaya ya Dodoma,
·        Wawakilishi wa Taasisi zisizo za Kiserikali,
·        Wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya malaria,
·        Waandishi wa Habari,
·        Mabibi na Mabwana.

Ndugu Wananchi,
Nichukue fursa hii ya awali kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kupata fursa siku hii ya leo na kuweza kuzungumza nanyi kuhusiana na maadhimisho ya siku hii muhimu ya Malaria Duniani kwa mwaka huu (2016).
Kwa kipindi cha miaka 15 sasa, Siku ya Malaria Duniani imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka hapa nchini tarehe 25 ya mwezi Aprili.

Kihistoria siku hii ilianzishwa baada ya Wakuu wa nchi za Afrika kukutana huko Abuja nchini Nigeria mwaka 2000 na kutoa Azimio la kuwepo na siku maalumu ya kukumbushana na kuelimishana kuhusu madhara yatokanayo na ugonjwa wa malaria na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali katika udhibiti ugonjwa wa huu. Tangu wakati huo, siku ya malaria duniani imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka hapa nchini. 

Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuwaelimisha wananchi ili watambue athari za ugonjwa wa malaria; wajue namna malaria inavyoambukizwa, na jinsi ya kujikinga. Aidha, maadhimisho haya pia hutumika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua dalili za malaria; na kuwahi mapema kituo cha kutolea huduma za afya, ili kupima na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kuanza kutumia dawa. Na iwapo mtu atathibitika kuwa na malaria, basi kutumia dawa na kuhakikisha kuwa anakamilisha matibabu ya malaria kulingana na maelekezo ya mtoa huduma. 

Ndugu Wananchi,
Bado takwimu kutoka katika vituo vya kutolea huduma zinaonesha kuwa takribani wastani wa watu milioni 12 hupata ugonjwa wa malaria kila mwaka hapa nchini. Makundi yanayoathirika zaidi ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano (5) na mama wajawazito. Ikumbukwe ugonjwa huu wa malaria  ni hatari kwa uhai wetu, maendeleo na ustawi wa Taifa letu, na ndiyo moja ya sababu kubwa inayochangia  katika kupunguza kasi ya maendeleo  ya jamii, hii ikiwa ni pamoja na kuleta vifo na madhara mengine yatokanayo na malaria. Jambo jema ni kuwa madhara haya yanaweza kupunguzwa na kutokomezwa kabisa kama tutatumia vizuri mikakati iliyothibitishwa katika kudhibiti ugonjwa wa Malaria hapa nchini.

 Ndugu Wananchi, 
Kutokana na utelekezaji wa mikakati ya udhibiti wa malaria hapa nchini kupitia wizara yangu, matunda yameanza kuonekana na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya malaria. Ripoti ya utafiti wa viashiria vya VVU/UKIMWI na Malaria inaonesha kuwa maambukizi ya malaria yamepungua kwa asilimia 50 kutoka asilimia 18 mwaka 2007/2008 hadi asilimia 10 mwaka 2011/2012. Pamoja na kupungua kwa maambukizi ya malaria, takwimu zinaonesha kuwa malaria bado ni tatizo katika maeneo ya vijijini ikilinganishwa na maeneo ya mijini ambapo maambukizi maeneo ya vijijini ni asilimia 10.7 na mijini ni asilimia 3.4. Kupungua kwa maambukizi ya malaria kunatupa kila sababu ya kujipongeza, na kumshukuru kila mdau aliyechangia kwa namna moja au nyingine katika jitihada hizi, ikijumuisha wadau wa maendeleo na mashirika ya kimataifa kwa kuwekeza katika mapambano dhidi ya malaria. Hata hivyo, bado tunayo kazi ya kufanya. Lengo ni kupunguza maambukizi ya malaria hadi asilimia 5. Mwaka 2016 na asilimia 1 ifikapo mwaka 2020. Hili linawezekana. Kila mmoja wetu anao wajibu wa kushiriki vita hii dhdi ya malaria.

Kipekee nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mhe. Dtk. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais mstaafu wa Awamu ya nne kwa jitihada zake nzuri za kupambana na malaria ndani na nje ya nchi na hadi kutunukiwa Tuzo iliyotukuka ya “White House Summit Award” mwezi Aprili 2016. Tuzo ni amepewa kutokana na kutambua jitihada na kutathimini mchango wake mkubwa na kubwa zaidi kwa kuwa mwanzilishi na kusimamia uanzishwaji wa muungano wa viongozi wa Afrika katika mapambano dhidi ya malaria “ African Leaders Malaria Alliance” (ALMA), muungano ambao hadi sasa una viongozi 49. Serikali ya Awamu ya 5 inampongeza sana na tunaahidi kumpa ushirikiano katika jitihada zake hizi njema.

Ndugu Wananchi,
Msisitizo mkubwa wa Wizara yangu ni kwa wananchi na wadau wote kuona umuhimu na kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya mikakati na afua zilizopo katika kuuthibiti ugonjwa huu. Iwapo mikakati hiyo itatekelezwa ipasavyo ni dhahiri kuwa maambukizi yataendelea kupungua kwa kiasi kikubwa na hatimaye kumaliza kabisa tatizo hili. Mikakati inayotekelezwa na Wizara  kwa kushirikiana na  wadau ni pamoja na:

1.   Udhibiti wa mbu; kwa kutumia njia mbalimbali, mathalani kwa kutumia vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu; unyunyuziaji wa viuatilifu ukoko katika kuta ndani ya nyumba; kusafisha mazingira na kuua viluwiluwi vya mbu kwa kutumia viuadudu vya kibailojia hasa katika maeneo ya mijini.

2.   Uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa malaria; kwa kuongeza kasi ya upimaji wa ugonjwa wa malaria kwa kutumia kipimo kinachotoa majibu kwa haraka (mRDT) au hadubini, na kutumia dawa mseto kama safu ya kwanza pale mgonjwa anapogundulika kuwa ana vimelea vya malaria; kuwapa wajawazito dawa ya kinga dhidi ya malaria kwa kutumia dawa ya Sulphadoxine Pyrimethamine (SP) kwa vipindi maalumu, na pia kuwapatia vyandarua vyenye viuatilifu wakati wa ujauzito.

Ndugu Wananchi,
Kwa sasa wananchi walio wengi wananufaika na mikakati na huduma mbalimbali za kupambana na malaria hapa nchini kama vile upatikanaji wa tiba sahihi ya malaria, vyandarua vyenye viuatilifu, upuliziaji wa viuatilifu ukoko katika kuta za nyumba katika Mikoa ya kanda ya Ziwa na matumizi ya viuadudu vya kibaiolojia katika sehemu zenye mazalia ya mbu, hasa katika maeneo ya mijini hususan Mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa upande wa vyandarua vyenye viuatilifu, siku hii ya Malaria Duniani kwa mwaka huu inaadhimishwa ikiwa tunajivunia hatua nzuri iliyofikiwa ya zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu katika kaya bila malipo. Zoezi hili ambalo lilianza rasmi mwaka jana, linalenga katika kugawa vyandarua vyenye viuatilifu nchi nzima, isipokuwa kwa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, ambayo inatekeleza mpango wa ugawaji vyandarua kupitia wanafunzi shuleni unaojulikana kama School Net Program (SNP).

Hadi sasa tayari zoezi hili limeshafanyika katika mikoa 18 ya Tanzania Bara, ambapo jumla ya vyandarua zaidi ya million 20 vimegawiwa kwa wananchi kwa uwiano wa chandarua kimoja kwa matumizi ya watu wawili. Utekelezaji wa kampeni hii unafanyika kwa awamu, na Mikoa iliyobaki ambayo haijagawiwa vyandarua ni Mikoa minne tu ya Dar-es-Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga. Tayari uandikishaji wa wanakaya katika mikoa hii umefanyika ili kupata idadi kamili ya vyandarua vitakavyohitajika. 

Wizara  inatoa msisitizo kwa wananchi kulala ndani ya chandarua kila siku ili kujikinga na maambukizi ya malaria kwani Serikali imetumia gharama kubwa kwa ajili ya kuvinunua na kusambaza kwa kila kaya. Kuwa na chandarua ni jambo moja na kutumia chandarua ni jambo jingine. Nitoe rai na hamasa kwa wananchi kutumia chandarua ili kujikinga na malaria.

Sambamba na ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu, Serikali kupitia Wizara yangu ikishirikiana na wadau, inatekeleza mkakati wa upuliziaji viuatilifu ukoko katika kuta za ndani ya nyumba. Mkakati huu unatekelezwa katika baadhi ya wilaya za mikoa ya Kanda ya Ziwa zenye maambukizi makubwa ya malaria. Kwa mwaka huu zoezi la upuliziaji limefanyika katika Halmashauri 8 za Musoma, Butiama, Ngara, Missenyi, Kwimba, Bukoba Vijijini, Chato na Sengerema. Jumla ya kaya 459,212 zimepuliziwa viuatilifu ukoko na kukinga takribani jumla ya wakazi 2,296,260.

Ndugu Wananchi
Kwa upande wa matibabu na vipimo (vitendanishi) vya malaria, wizara yangu imeendelea kuhakikisha kuwa tiba sahihi inatolewa kwa wagonjwa wa malaria; hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa vipimo vya kutambua uwepo wa vimelea vya malaria kwa kutumia hadubini au kipimo kinachotoa majibu ya haraka (mRDTs) vinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya wakati wote. Aidha, vipimo vinafanyika kwa utaalamu, na dawa kutolewa kwa wale tu wanaothibitika kuwa na vimelea vya malaria.  Kwa sasa vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya Serikali hapa nchini vinapima malaria kwa kutumia aidha hadubini au mRDTs. Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa wataalamu wanapatiwa mafunzo mbalimbali ili kuboresha utaalamu na weledi. Kwa kupitia juhudi hizi za Wizara yangu, kumekuwepo na ongezeko la upimaji kufikia asilimia 83 katika vituo hivyo; kiasi ambacho kinazidi lengo ambalo Wizara ilijiwekea la  angalau asilimia 80.

Kwa upande wa vituo vya huduma za afya kutoka sekta binafsi, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imetoa mafunzo kwa mafundi sanifu wa maabara kutoka takribani asilimia 60 ya vituo vyote vilivyosajiliwa na Wizara kwa sasa, ambavyo vipo katika mikoa 8 ya Tanzania bara. Mikoa hiyo ni pamoja na Dar-es-Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Mbeya, Tanga, Arusha na Mwanza. Kwa Mikoa mingine iliyobaki, mafunzo yatakamilishwa katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017. Lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa huduma za upimaji zinapatikana pia katika sekta binafsi ambayo, kwa mujibu wa utafiti ngazi ya jamii (THMIS) wa mwaka 2011/12, sekta hii inahudumia takribani asilimia 40 ya watanzania wote. Natoa msisitizo kwa wananchi kuwa iwapo itatokea kupata dalili za homa, tuhakikishe kuwa tunawahi katika kituo cha kutolea huduma za afya, kisha tupime na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kuanza  matibabu.

Ninapenda niwahakikishie wadau wa sekta binafsi wanaotoa huduma za afya kwamba, Wizara yangu inaendelea na jukumu la kuwawezesha watoa huduma wote ili watoe huduma ya afya kwa mujibu wa Kanuni, miongozo na taratibu zilizowekwa na Wizara. Ikumbukwe kwamba sera ya afya ni moja; na mwongozo wa matibabu na upimaji wa malaria ni mmoja.

Sambamba na vipimo, wizara yangu pia inahakikisha kuwa dawa zenye usalama, ubora na ufanisi za kutibu malaria zinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini (serikali na binafsi). Kwa upande wa vituo vya serikali pamekuwepo na ongezeko la upatikanaji wa dawa za kutibu malaria na kuwafikia wananchi kwa urahisi. Upungufu wa dawa za malaria uliokuwepo umepungua kwa kiasi kikubwa katika vituo kutoka asilimia 25 iliyokuwepo mwaka 2012 hadi asilimia 6 tu hivi sasa.

Serikali pia inashirikiana na wadau katika mpango wa utoaji wa dawa mseto za malaria kwa bei ya punguzo kupitia sekta binafsi kwa kujumuisha  vituo vya kutolea huduma za afya vya binafsi na maduka ya dawa. Hii inalenga kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi atakayekosa dawa za malaria pale anapougua. Kupitia mpango huu unaojulikana kama Co-Payment Mechanism, ambao unatekelezwa nchi nzima, wananchi wanaweza kununua dawa za malaria kwa bei nafuu kabisa, toka maduka ya dawa binafsi.

Tukumbuke kuwa mazoea ya kutumia dawa bila kupima yamepitwa na wakati; kwani si kila homa ni malaria. Utafiti uliofanywa mwaka 2012 wa kutambua sababu za homa hapa nchini kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10, unaonesha wazi kuwa asilimia 62 ya watoto waligundulika kuwa na homa, homa hizo  zilisababishwa na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa, wakati waliokutwa na malaria walikuwa ni asilimia 10.5 tu. Hii inaendelea kuthibitisha kuwa sio kila homa ni malaria.

Hivyo basi, tunasisitiza na kuhimiza wananchi kupima na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kuanza kutumia dawa. Na pale watakapogundulika kuwa wana malaria, basi wahakikishe wanatumia dawa na kumaliza kozi nzima ya dawa, kulingana na maelekezo ya mtoa huduma.

Ndugu Wananchi,
Ni muhimu pia kwa wanajamii kushiriki kikamilifu katika kuharibu mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji, kusafisha mifereji na kuweka mazingira safi ili kuondoa maji yaliyotuama, na hivyo kuchangia katika kupunguza maambukizi ya malaria.

Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya kutoka nchini Cuba (LABIOFAM) imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha viuadudu (biolarvicides) ambavyo vitatumika kuua viluwiluwi vya mbu katika mazalia (madimbwi, mabwawa na sehemu nyingine zinazozalisha mbu). Kiwanda kipo katika hatua za mwisho kuanza uzalishaji wa viuadudu. 

Ndugu Wananchi,
Mapambano dhidi ya malaria yanahitaji juhudi za pamoja kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wanaoshughulika na udhibiti wa Malaria. Napenda nichukue fursa hii kwa niaba ya Serikali, kutoa shukrani zangu za dhati kwa wadau wetu; Mfuko wa Dunia wa kushughulikia ugonjwa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (The Global Fund), Mfuko wa Rais wa Marekani wa kushughulikia Malaria (PMI), Shirika la Misaada la Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la UNITAID, Taasisi zisizo za Kiserikali, Sekta binafsi kupitia Mpango wa Malaria Safe, Taasisi za utafiti (NIMR na Ifakara Health Institute)  nikitaja kwa uchache; na bila kuwasahau wananchi katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla kwa kuwa tayari kutumia mikakati hiyo.

Ndugu Wananchi,
Nimalizie kwa kusisitiza kwamba iwapo tutaitekeleza ipasavyo mikakati niliyoitaja hapo juu, ninaamini kuwa ugonjwa wa malaria utakuwa si tatizo tena katika jamii yetu. Tunaweza kabisa kujikinga na ugonjwa wa malaria, na pia ugonjwa wa malaria unatibika na kupona kabisa iwapo mgonjwa atawahi kupata tiba sahihi mara tu baada ya kuanza kwa dalili, na kukamilisha kozi nzima ya dawa ya malaria kulingana na maelekezo ya mtoa huduma.     

Ili kuendeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana, katika jitihada za kutekeleza mikakati muhimu, tunahitaji kuongeza juhudi zaidi, kutenga rasilimali fedha zaidi kwa kushirikiana na wadau wote, ili tuweze kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria hapa nchini kwa manufaa ya jamii nzima.
Nachukua fursa hii kusisitiza yafuatayo kwa wanajamii:
·        Kuzingatia kupima ili kujua uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kutumia dawa.
·        Kumaliza kozi ya dawa kulingana na maelekezo ya mtoa huduma.
·        Kutumia vyandarua vyenye viuatilifu kila siku wakati wa kulala.
·        Kuzingatia usafi wa mazingira kuzuia mazalia ya mbu.

Kwa upande wa halmashauri zote nchini nasisitiza yafuatayo:
·        Kuboresha takwimu ili kujua ukubwa wa tatizo la malaria katika Halmashauri zao.
·        Kuhakikisha kwamba wanaweka bajeti kwenye mipango yao ya Halmashauri (CCHP) kwa ajili ya udhibiti wa mbu.
·        Kuhakikisha miongozo ya uchunguzi na tiba ya malaria inazingatiwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya umma na vya sekta binafsi.
·        Kufanya ufuatiliaji katika vituo vya kutolea huduma vya umma na vya sekta binafsi ili kuboresha huduma.

Mwisho kabisa niwakumbushe kuwa zama zimebadilika “Sio kila homa ni Malaria nenda ukapime”, na “lala kwenye chandarua kila siku” kujikinga na malaria.  

                            ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.


Matukio mbali mbali ya picha katika maadhimisho ya siku ya malaria duniani ambapo Waziri wa Afya nchini Ummy Mwalimu wakiwemo baadhi ya waandishi wa habari wameiadhimisha siku hii kwa Kupima Malaria kwa kutumia kipimo cha haraka(mRDT)

Waziri wa afya,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto Ummy Mwalimu akiwaonesha waandishi wa habari kipimo cha haraka cha kupima malaria(mRDT) wakati akitoa tamko la maadhimisho ya siku ya malaria Duniani leo kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma

Kulia ni mkuu wa kitengo cha udhibiti wa mmbu waenezao malaria charles dismas kutoka mpango wa Taifa wa kudhibiti malaria.
Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria,Dkt.Renata Mandike(kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusiana na utekelezaji wa udhibiti wa malaria nchini
Baadhi ya wataalam wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma pamoja na waandishi wa habari wakimsikiliza waziri Ummy Mwalimu
Fundi sanifu maabara Habiba Malima akimchukua damu waziri wa afya,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto kwa kipimo cha malaria Rapid Diagnosist Test(mRDT),kipimo hicho ni cha haraka na huchukua dakika ishirini kugundua kama una malaria,kipimo hiki kilianza kutumika nchini mwaka 2009
Waandishi wa habari wakiwa wamejipanga mstari tayari kwa kupima malaria
Mwandishi wa habari kutoka clouds media Kijah Yunus akipima malaria

Ijumaa, 8 Aprili 2016

Waziri wa Afya Mh.Ummy Mwalimu azindua duka la dawa kandaa ya mbeya!

Mh.Ummy Mwalimu akipata maelezo jinsi ya
 utunzaji dawa kwenye ghala hilo
Duka la dawa la Bohari kuu ya dawa(MSD)kanda ya mbeya ambalo litahudumia mikoa ya Mbeya,Rukwa na Katavi 

Mh.Ummy Mwalimu akionesha moja ya dawa inayouzwa dukani hapo kwa shilingi 7,000 ambapo kwenye maduka binafsi inauzwa shilingi 25,000,kushoto ni mkurugenzi mkuu wa MSD Laurine Bwanakunu na kulia ni
 Mfamasia wa duka hilo Cornel Mkeng'e


Mfamasia wa duka la dawa Cornel Mkeng'e akitoa aelezo kwa Mh.Ummy Mwalimu mara baada ya kuzindua duka hilo

Waziri wa afya Mh. Ummy Mwalimuakiangalia jinsi 
ya ufungashaji wa dawa  kwenye ghala jipya la kanda 
ya mbeya ambalo limezinduliwa leo jijini hapa na Mh.Ummy Mwalimu 


Duka hili la dawa kanda ya mbeya  limetumia shilingi milioni.13 kwa ukarabati kwa jengo na vifaa vyake.


Alhamisi, 7 Aprili 2016

MAGONJWA 10 YA KURITHI AMBAYO NI MUHIMU KUPIMA AU KUYAJUA NA MPENZI WAKO KABLA YA KUZAA MTOTO.


Magonjwa ya kurithi ni yapi?
Haya ni magonjwa ambayo yapo kwenye koo za watu fulani na hurithiwa kutoka kizazi mpaka kizazi lakini pia magonjwa haya huweza kutoka kwa mwanamke na mwanaume ambao kwa macho ni wazima kabisa na kuzaa watoto wenye matatizo ya kiafya.

Kwenye jamii zetu za kiafrika ni jambo la kawaida sana kuzaa tu bila kupima kujua kama kuna hatari ya kuzaa mtoto mwenye matatizo makubwa ya kiafya kutokana na vimelea vya kurithi yaani DNA ambazo wazazi husika wamezibeba, mimba nyingi zimekua zikisingiziwa kwamba hazikupangwa na wakati kila mtu anajua mwisho wa ngono zembe bila njia yeyote ya uzazi wa mpango ni mimba.
Hii ni tofauti na nchi zilizoendelea ambapo wazazi hupima vipimo hivi kabla ya kuamua kuzaa na hata ikigundulika mtoto anayekuja atakua na matatizo mimba hiyo hutolewa ili kuepusha maumivu ambayo mtoto huyo angeyapata kama angezaliwa na maumivu ya kisaikolojia na kiuchumi ambayo wazazi wanaozaa watoto kama hawa wanayapata, hii ni kwasababu ya kulazwa mara kwa mara kwa mtoto husika na kushindwa kufanya kazi maisha yake yote.

Hivyo nchi zilizoendelea watoto wanaozaliwa na magonjwa ya kurithi wametokomezwa kwa kiwango kikubwa sana tofauti na afrika ambapo watoto hawa ni wengi sana na kila siku wanazidi kuzaliwa, wakati wangeweza kuzuilika kama sisi wahusika na serikali ingechukua hatua kukomesha hili kwa kuingiza vifaa vya kitaalamu ya kuyagundua magonjwa haya muhimu.
Ni kweli vipimo vingi havipatikani hasa maeneo ya vijijini na hata mijini lakini kuna watu ambao wako kwenye nafasi kubwa ya kuzuia na kupunguza idadi ya watoto hawa wanazaliwa kila siku, hasa watu wanaoishi mijini na wenye uwezo kifedha lakini hata wewe ambaye huwezi kupata vipimo hivi hebu jaribu kwenda ukweni kwa mumeo au mkeo unaweza ukaona ugonjwa wa kurithi ambao sio wa kawaida huko na kufanya maamuzi vizuri au unaweza ukamuuliza mumeo au mkeo ili awe muwazi kabla ya kufunga ndoa kwani magonjwa mengine yanaonekana kwa macho tu.
Magonjwa haya ni kama yafuatayo


1.Sickle cell disease;{siko seli] huu ni ugonjwa wa kurithi ambao mtoto hurithi kutoka kwa baba na mama ambapo wazazi wawili ambao wanakua hawana dalili yeyote hubeba ugonjwa huu kwenye damu zao yaani carrier na wanakua na uwezekano wa 25% ya kumzaa mtoto huyu ambae ataugua na kua na dalili zote za ugonjwa huu. Ugonjwa huu ni hatari sana. Mwaka 2013 ugonjwa huu uliua watu laki mmoja na elfu sabini na sita duniani kote wengi wakitokea Africa hasa chini ya jangwa la sahara. Watoto hawa huanza na dalili za kuvimba vidole wakiwa na umri wa miezi mitatu, kuvimba vichwa, kua na miguu na mikono mirefu na miembamba, kulalamika maumivu makali, kuishiwa damu sana  na kadhalika ukubwani. Kama wapenzi wakipimwa wakakutwa wote wameubeba ugonjwa huu kwenye damu zao yaani carriers ni vizuri wakaairisha ndoa hiyo kwani watakaribisha matatizo makubwa kwenye maisha yao. Kama unataka kujua umebeba ugonjwa huu ukienda hospitali kubwa za rufaa wana uwezo wa kuwapima na kujua. Ugonjwa huu pia unaweza kupimwa kwa kuchukua maji kwenye tumbo la mama kabla hajazaliwa hivyo kuamua kuendelea na mimba au kuitoa. Japokua kutoa ni kosa kisheria nchini Tanzania. Watoto hawa huishi kwa mateso makali na 50% watakufa kabla ya miaka 40 kwa nchini kwetu Tanzania hakuna data kamili za watu hawa lakini wasichana wengi wenye ugonjwa huu hufa wanapoanza kuziona siku zao kwani damu hupungua zaidi na viungo vingi kushindwa kazi.

2.Haemolytic diseases of the new born;  kuna aina kuu nne za group za damu yaani A, B, AB, na O ambazo group hizo mtu anaweza kua positive au negative mfano mtu mwingine anaweza kua A positive na mwingine akawa  A negative au B positive na mwingine B negative.Sasa swala ni kwamba watu wa negative wakioana hakuana shida au watu wa positive wakioana hakuna shida LAKINI mwanaume wa positive akioa mwanamke wa negative mtoto wa kwanza atazaliwa vizuri lakini ataacha vitu vinaitwa antibodies ambavyo kazi yake itakua ni kuharibu mimba zote zitakazofuata kutoka kwa mwanaume huyu. Kipimo hichi ni rahisi sana na kinapatikanakaribia hospitali zote Tanzania na hata kama mmeshaoana tayari na mna tatizo hili kuna dawa maalumu inaitwa RHoGAM mama mjamzito anachomwa wiki ya 28 mpaka 32 kuzuia vifo hivyo.
 3.Albinism{Ualbino]: huu ni ugonjwa wa kurithi ambao motto huzaliwa bila vimelea vya melanin au kua na uchache wa vimelea hivyo ambavyo humfanya mtu apate rangi ya ngozi yake. Mara nyingi wazazi wote wawili wa mtoto huyu hubeba ugonjwa huu kwenye miili yao bila kua na dalili yeyote na wao kumzaa mtoto ambaye ni albino lakini pia kuna aina za ualbino ambazo mzazi mmoja anaweza kusababisha albino kuzaliwa bila mama kua na vimelea vya ualibino.Mtoto huyu huzaliwa akiwa na matatizo ya kutoona vizuri na makengeza, ngozi na nywele nyeupe sana. Kua albino sio ugonjwa lakini watu hawa hua kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kansa ya ngozi. Sio rahisi kupima kujua kama mtu anabeba vimelea vya ualbino kwenye mwili wake lakini inawezekana kupima mtoto aliyeko tumboni na kugundua kama nia albino au sio kwa nchi zilizoendelea au unaweza kumjua mwenzako kwa kuona albino kadhaa kwenye ukoo wao.
 4.Magonjwa ya akili: katika jamii kuna watu hua wanafanya vitu ambavyo sio vya kawaida mpaka unajiuliza huyu mtu amechanganyikiwa au vipi..yaani ni mtu wa fujo, hajifunzi kwa makosa ya nyuma, unasikia mtu kamuua mzazi wake,anavunja sheria mara kwa mara, kunywa pombe sana, anakasirishwa na vitu vidogo sana au maisha yake ya mahusiano yanakua ni ya ugomvi kila siku yaani kwa kifupi anakua tofauti na wengine. Dalili hizi sio za kupuuzia kuna uwezekano mkubwa sana wa kuzaa watoto wa aina hii ambao huanza kusumbua tangu wakiwa shule ya msingi na kupata matatizo makubwa ukubwani. Shida hizi hazihitaji vipimo ni wewe kutoa maamuzi mapema kabla hamjaamua kuzaa naye kwani mambo hayo yanarithiwa na mimi nimeshashuhudia familia nzima ya watu waliokua hawana akili nzuri yaani walikua wehu kabisa.
5.Magonjwa ya kansa; ugonjwa wa kansa haurithiwi lakini kuna baadhi ya koo zina vimelea{genes] ambazo baadae husababisha kansa. Ni vizuri kujua vyanzo vya vifo vya ndugu wa mwenza wako kabla ya kuamua kuzaa naye kwani ugonjwa huu unaweza kua ni mbaya zaidi kuliko magonjwa yote ya kurithi. Kuna familia naifahamu nyumba ilifungwa kwani watu wote waliuawa na kansa yaani mume na watoto wote waliozaliwa, dada na kaka wote wa mume isipokua mke tu aliyekua ameolewa pale.
6.Ugonjwa wa kisukari; ugonjwa huu yaani diabetes mellitus type 2 unawapata sana wagonjwa watu wengia ambao kwao kuna ugonjwa huu. Yaani kama baba yako na mama yako wana kisukari uwezekano wa wewe kupata kisukari ni asilimia hamsini. Maana yangu ni kwamba ukioa au ukiolewa na mtu ambao kwao kuna wagonjwa wa kisukari ujue kuna uwezekano wa mtoto wenu mmoja kuugua ugonjwa huo miaka ya baadae. Hivyo hua tunashauri kama wazazi wako wana kisukari kuepuka kua mnene kwani utakikaribisha mapema.
7.Ugonjwa wa asthma au pumu; ugonjwa huu ambao hushambulia mfumo wa upumuaji hufuata sana ukoo fulani wa watu japokua pumu zipo za aina mbili ile ya kurithiwa na ile ambayo sio ya kurithiwa hivyo kama ukoo unaoenda kuoa au kuolewa una wagonjwa wawili au watatu wa asthma kuna uwezekano mkubwa sana wa kumzaa mtoto mwenye pumu baadae, ugonjwa ambao huua haraka kama usipopata ufuatiliaji wa kutosha
8.Ugonjwa wa kifafa; japokua ugonjwa hu huweza kusababishwa na magonjwa mengine kama homa ya uti wa mgongo, ulaji wa nyama ya nguruwe na kadhalika ugonjwa huu umeonekana kufuata koo Fulani za watu yaani kama unaenda kuoa kwenye ukoo ambao unafahamu kuna wagonjwa wa kifafa uwezekano wa kuzaa watoto wenye kifafa upo hivyo ni vema kuingia unajua.
 9.Umbilikimo: huu ni ugonjwa wa kurithi ambao watu wanazaliwa sana kitaalamu unaitwa achondroplasia, wazazi wa watoto hawa ambao hua na mikino na miguu mifupi sana huweza kua kawaida kabisa lakini kutokana na kurithi vimelea vya ugonjwa huu hujikuta wanamzaa mtoto huyu na mtoto huyu baada ya muda Fulani akioa anazaa mtoto wa hivi hivi kwani mzazi mmoja tu huweza kusababisha hali hii.
 10.Magonjwa ya upofu; kuna koo ambazo watoto huzaliwa na vimelea vya hali ambayo husababisha upofu baadae au ikasababisha upofu hata kabla ya mtoto kufikisha miaka mitano. Mtoto huzaliwa na mtoto wa jicho kitaalamu kama congenital cataract ambayo huziba jicho taratibu na baadae mtu hataona kabisa na unaweza ukakuta ukoo una vipofu wengi na chanzo husika hakifahamiki.
Mwisho; haya ni baadhi ya magonjwa ambayo labda yameathiri watu wengi kwenye jamii zetu lakini yapo mengine mengi ambayo siwezi kuyataja na  makala hii haijaandikwa kuwatenga au kuwasema vibaya watu wenye matatizo haya kwamba wasioe au wasiolewe lakini ni kujaribu kuongea ukweli na kuepusha watu wenye tatizo moja kuzaa mtoto kwani ni kujiongezea matatizo tu kama nilivyosema hapo mwanzoni na kuleta viumbe ambavyo vinakuja duniani kuteseka sana. 

Ni bora waendelee kuzaliwa carriers yaani wanaobeba vimelea bila kuugua kuliko kuendelea kuwazaa wagonjwa.hivyo kama wewe unajua kwenu kuna shida fulani ni bora kuzaa na mtu ambaye kwao hamna shida kabisa kwani ukizaa na mtu mwenye matatizo kwao pia ni hatari zaidi na kama ukiamua kukaidi na  kuzaa hivyohivyo uzae unajua kwamba haya magonjwa yapo. niwape pole ambao tayari ni wagonjwa wa hali hizi na wale wenye ndugu wenye hali hizi.dunia inatambua maumivu yenu.

DAWA ZA NYWELE ZINAZOSABABISHA UVIMBE WA KIZAZI KWA WANAWAKE




Dawa za kulainisha nywele (relaxer) zimekuwa zinapendwa na wanawake wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na kumfanya apendeze na awe wa kuvutia.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinasababisha uvimbe kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo ambazo huingia mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.

 
Daktari wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata alifanya utafiti na kubaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye kizazi uitwao fibroids au leimyoma.

 
“Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata kwa harufu tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya estrogen ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa fibroids,” anasema.

Dk Chipata anasema kukua kwa uvimbe kwenye kizazi hutokea katika kipindi ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.

Utafiti wa Dk Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha wanawake wa kada tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.

 
“Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvinbe kwenye kizazi, zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na za kwenye mafuta ya ngozi kama vile mercury na hydroquionone,” anasema.

Dk Chipata anasema madhara yanayopatikana katika kemikali za vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha saratani au kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya zebaki (mercury).

 
“Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi baada ya mtu kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye ngozi kutokana na mfumo wa ngozi,” anasema.

Anashauri kuwa ni vyema watu wakasoma kipodozi kimetengenezwa kwa nini kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi kubaki na ngozi au nywele halisi badala ya kujibadilisha.

 
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye kemikali kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinyl chloride, zirconium na bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.

Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dk Lauren Wise na wenzake nchini Marekani na kuchapishwa kwenye jarida la afya la nchini Marekani ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au vivimbe hivi hujulikana kama fibroids au myoma.

 
Dk Wise anasema aliwafanyia uchunguzi wanawake wanaotumia dawa za kulainisha nywele na kuangali umri walioanza kutumia dawa hizo, mara ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa kipindi gani.

Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa upasuaji.

 
Kwa nini relaxer ni hatari kwa wanawake?
Dk Wise anasema mchanganyiko ulio kwenye dawa za nywele hasa zilizoandikwa “Lye Relaxer” ni sodium hydroxide wakati makopo ya dawa yaliyoandikwa “No Lye Relaxer” yana calcium hydroxide na guanidine carbonate.

Bidhaa za kulainishwa nywele zilizoandikwa ‘no lye relaxer’ zinadaiwa kusababisha majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha na zile zilizoandikwa “Lye Relaxer”.