Na
Emmanuel Lengwa, Mbozi
mtoto Bahati akiwa amelala katika chumba ambacho alifungiwa |
Muandishi Emmanuel Lengwaakiwa na mtoto Bahati Kaminyonge, baada ya kumtoa katika chumba alichokua amefungiwa |
Mwanamke mmoja
anashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilayani Mbozi kwa tuhuma za kumfanyia ukatiri
wa kutisha mwanae wa kuzaa kwa kumfungia ndani ya nyumba kwa miaka kumi bila
kumpatia baadhi ya huduma muhimu.
Mkuu wa Wilaya Mbozi
Ahamed Namohe alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Irene Mwamlima ambaye ni mama
mzazi wa mtoto Bahati Kaminyoge (12) anayedaiwa kufanyiwa ukatiri huo.
Akizungumzia suala hilo,
Namohe alisema kuwa Wilaya yake imekuwa na matukio mengi ya ukatiri wa watoto,
lakini hayaripotiwi kwenye vyombo vya dola ili yafanyiwe kazi.
Namohe alisema kuwa
Mwamlima na mumewe aitwaye Ally Kaminyoge wanadaiwa kumfungia mtoto huyo ndani
ya nyumba bila kumpatia huduma kama vile malazi mazuri, chakula cha lishe bora
na mavazi, hali ambayo alidai kuwa ni ukatiri mkubwa dhidi ya mtoto huyo.
“Mtoto huyo amefanyiwa
ukatiri wa kupitiliza na jambo baya zaidi ukatiri huo unafanywa na wazazi wake,
matukio haya ni mengi lakini hayaripotiwi, hivyo nitoe wito kwa wananchi kutoa
taarifa za ukatiri wa aina hii ili Serikali iweze kuchukua hatua,” alisema
Namohe.
muandishi alifika
nyumbani kwa Kaminyonge katika nyumba alimokuwa amefungiwa mtoto huyo, na
kushuhudia mtoto Bahati akiwa amelazwa chini sakafuni, huku akiwa hana nguo
zaidi ya blanketi dogo ambalo hujifunika usiku na mchana kujikinga na baridi.
Aidha kutokana na
kutoruhusiwa kutoka nje mtoto huyo alikuwa akijisaidia ndani ya chumba
alichofungiwa, hali iliyosababisha aishi katika mazingira machafu, yenye wadudu
na harufu kali.
Akizungumzia
suala hilo, Mwenyekiti wa Kituo cha Haki za Binadamu mkoani Mbeya, Said Mohamed
alisema kuwa alipata taarifa za kufungiwa ndani kwa mtoto huyo kutoka kwa
wasamalia wema na akaamua kuchukua hatua za kuishirikisha Serikali kwenda
kumwokoa mtoto huyo.
Alisema kuwa hali
aliyoishuhudia kwa mtoto huyo inatisha na kwamba kutokana na ukatiri huo ni
lazima wazazi wa mtoto Bahati wachukuliwe hatua za kisheria ili kutoa fundisho
kwa watu wengine.
“Ukatiri aliofanyiwa
mtoto huyu na wazazi wake hauvumiliki, maana tumemkuta mtoto huyu akiwa ni kama
ametupwa kwenye dampo la taka, akiwa hana nguo na amelala sakafuni huku akiwa
amejifunika blanketi chafu linalotoa harufu kali ya vinyesi, katika hili ni
lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wazazi hawa,” alisema
Mohamed.
Mama mzazi
wa mtoto huyo, Irene Mwamlima alisema kuwa mwanaye huyo alizaliwa akiwa na
uzito mdogo na baada ya miezi mitatu alibainika kuwa hakui tena!
Alisema kuwa
alipompeleka hospitali, aliambiwa kuwa mwanaye huyo ana ulemavu wa akili, hali
ambayo ilimlazimu sasa waanze kumfungia ndani kwa madai kuwa akiachwa huru
atapotea!
Afisa Maendeleoya Jamii
Wilaya ya Mbozi, Edwin Kabambagusha alisema kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji
mkubwa wa sheria na haki za watoto, hivyo ni muhimu
jamii nzima ikaungana kuvikemea kwenye maeneo yao.
Alisema kuwa mtuhumiwa
huyo atafikishwa mahakamani kwa kuvunja sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2007,
huku akiitaka jamii kuepuka vitendo vya aina hiyo kwa kuwa ni kinyume cha
sheria.
Mama mzazi wa mtoto huyo
anashikiliwa kwenye kituo kikuu cha Polisi wilayani Mbozi cha Vwawa, akisubiri
kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ukatiri dhidi ya mwanae.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni