Utangulizi
Mheshiwa Waziri
Kwanza tunakupongeza kwa uamuzi wako wa kutembelea wadau wa wizara yako na kufika hadi kwetu sisi tulio pembezoni mwa nchi yetu kwa ajili ya kutusikiliza na pengine hata kufanyia kazi mawazo yetu kwa lengo la kuijenga nchi yetu.
Sisi kama wanahabari wa mkoa wa mbeya tumefarijika sana kwa ujio wako na tunaamini katika ziara yako mkoani mwetu utajifunza mengi ambayo yanaweza kuwa chachu kubwa ya maendeleo ya Tasnia ya Habari nchini kote.
Mheshimiwa Waziri,
CHAMA cha Wandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya (Mbeya Press Club) ni taasisi ya waandishi wa habari wa mkoa wa Mbeya, ambayo ilianzishwa tangu mwaka 1995 ikiwa ni taasisi yenye lengo la kuwa kitovu cha wanahabari katika kutafiti na kuandika habari zenye weledi na kutukutanisha pamoja, kupata mafunzo kwa kubadilishana ujuzi, uzoefu na uwezo ili kuboresha taaluma ya Uandishi wa Habari.
Kutokana na uwepo wa Mbeya Press Club, taaluma ya habari imekua kwa kiwango kikubwa mkoani Mbeya na hata hali ya ufikishaji wa taarifa kwa wananchi imekuwa bora na kwa kiwango cha hali ya juu.
Mheshimiwa Waziri
Wandishi wa Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa wanataaluma wanaojituma kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi wa hali ya juu na ndio sababu mkoa wetu umekuwa ukitambulika ndani na nje ya nchi kutokana na kutangazwa vema na sisi wanahabari.
Habari nyingi zinazoandikwa na wanahabari wa mkoa wa Mbeya zimekuwa ni chachu kubwa kwa maendeleo ya wakazi wa mkoa wetu na hata maeneo mengine kutokana kuandikwa kwa umahili mkubwa na wakati mwingine hata kuwa elimu kwa wanataaluma wa mikoa mingine nchini.
Mheshimiwa Waziri
Pamoja na kazi kubwa tunayoifanya wanahabari wa Mkoa wa Mbeya, lakini pia tunakabiliana na changamoto nyingi, lakini baadhi ya changamoto hizo zikiwa ni zile zinazowakabili wanahabari wote nchini.
Changamoto kubwa ya wanahabari wa Mkoa wa Mbeya ni kutumikishwa na wamiliki wa vyombo vya habari kwa muda mrefu bila ya kuwa na mikataba ya ajira sambamba na ujira kidogo tunaolipwa na wamiliki hao wa vyombo vya habari.
Tunatambua kuwa huwenda suala hili la wanahabari kupewa mikataba ya ajira likawa nje ya wizara yako, lakini kwa kuwa Serikali yetu ni moja, tunakuomba ujaribu kulishughulikia kwa kadri ya uwezo wako ikiwa ni pamoja na kukaa na wamiliki wa vyombo vya habari kuwashauri kumaliza tatizo hili sugu la wanahabari walio wengi hasa sisi tunaoishi pembezoni mwa nchi.
Mheshimiwa Waziri,
Hili la mikataba ya ajira kwa wandishi wa habari tumelileta kwako kwa sababu tunajua wewe kazi yako ni kusimamia tasnia hii ukihakikisha kuwa wanahabari wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi na maadili ya taaluma yao.
Ukweli ni kwa mba ni vigumu kwa wanahabari kuifuata misingi na maadili hayo kama maslahi yao ni duni na hawana mikataba ya ajira kutoka kwa waajiri wao.
Mheshimiwa Waziri,
Lipo tatizo kubwa la kuporomoka kwa maadili na misingi ya taaluma ya habari nchini, pia tunatambua kuwa wewe ndiye mwenye dhamana ya kusimamia ubora na maadili ya wanahabari, hivyo basi tunaomba japo kwa kifupi kuelezea kuwa chimbuko la tatizo hili ni uwepo wa utitiri wa vyuo vinavyotoa taaluma ya habari ambavyo havina sifa ya kutoa taaluma hiyo.
Vipo vyuo ambavyo vimesajiliwa kwa ajili ya kutoa taaluma ya upishi na utalii, lakini na vyenyewe vimejiingiza katika fundisha taaluma ya habari, jambo ambalo linapelekea kushusha heshma ya taaluma yetu ya uandishi wa habari.
Kwa kuwa wewe ndiye waziri unayesimamia tasnia hii, tunapenda kukushauri kulitupia jicho suala hili na kuweka mfumo wa kuvibaini vyuo vya aina hiyo na kuamuru wenye navyo waviboreshe au ikibidi uvifute ili vibakie vyuo vinavyotoa taaluma yenye ubora unaokubalika.
Mheshimiwa Waziri,
Suala lingine ambalo leo tungependa kupata ufafanuzi kutoka kwako ni mkwamo wa Muswada wa Sheria ya vyombo vya Habari ambao kwa miaka mingi umekwama kupelekwa bungeni ili vyombo vya habari viweze kupata sheria moja inayovisimamia.
Tunatambua kuwa mara kadhaa wamiliki wa vyombo vya habari nao wamekuwa kikwazo kikubwa kwa muswada huo kupelekwa bungeni, lakini sisi wanahabari wa Mkoa wa Mbeya tunaamini kuwa wamiliki wa vyombo vya habari nchini hawapendi Muswada huo upelekwe bungeni kwa ajili ya kulinda maslahi yao na siyo maslahi ya wandishi wa habari!
Tunasema hivyo kwa sababu Muswada wa vyombo vya habari umeainisha mambo mengi yenye maslahi kwa wandishi wa Habari, ambayo ukipitishwa utawalazimu wamiliki wa vyombo vya habari kuwatimizia wandishi wa habari matakwa yao ipasavyo na hivyo wao kuona kuwa watapatapa faida kidogo ikilinganishwa na wakati huu ambapo muswada huo haujapitishwa.
Mheshimiwa Waziri
Tunatambua yapo mambo yanayowafanya wamiliki wa vyombo vya Habari nchini kujenga hoja za kupinga muswada huo, kama vile vyombo vya habari vya watu binafsi kujiunga na Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) wakati wa taarifa ya habari ya saa 2 usiku.
Kwa mtazamo wetu madai hayo ya wamiliki wa vyombo vya habari yanazungumzika na yanaweze kurekebishwa na wabunge kabla ya muswada huo kupita hivyo, madai yao isiwe sababu ya kukwamisha muswada huo usipelekwe bungeni katika kipindi hiki cha uongozi wako.
Sisi tunaamini kuwa mwarobaini wa changamoto za wandishi wa Habari wa Mkoa wa Mbeya na kwingineko nchini ni kupelekwa kwa muswada huo bungeni upitishwe na kuwa sheria ambayo itasaidia sana kumaliza changamoto zetu.
Mheshimiwa Waziri
Pia kuna changamoto ya baadhi ya watendaji wa Serikali na maofisa Uhusiano wa Taasisi za umma kutotoa ushirikiano wa kutosha kwa wanahabari wanapofika kwenye maeneo yao kwa ajili ya kupata habari.
Tunakuomba ukiwa Waziri mwenye dhamana, kuwakemea maofisa hawa wachoyo ili waachane na tabia hiyo na badala yake watoe habari za maeneo yao kwa wanahabari tena kwa wakati.
Mheshimiwa Waziri tunakuomba ikiwezekana uwaagize maofisa Uhusiano wa taasisi za umma kutoa habari za viongozi hasa wa kiserikali kwa wanahabari punde tu habari hizo zinapojitokeza badala ya kusubiri wanahabari wenyewe ndio waende kuzitafuta kwenye ofisi zao.
Hitimisho
Mheshimiwa Waziri,
Nimalizie risara yetu kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kukuteua wewe kuwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia tasnia yetu akiamini kuwa unatosha na utaweza kuikwamua taaluma yetu hapa ilipo na kuisukumba mbele zaidi. Kwa mantiki hiyo pia tunaamini kuwa changamoto zetu utazifanyia kazi kwa nguvu zako zote na hatimaye taaluma ya Habari iweze kuboreka zaidi kwa manufaa ya wananchi.
Imendaliwa na Mbeya Press Club
Asante.
Mwisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni