JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO
TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU (MB) - WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MALARIA DUNIANI
TAREHE 25 APRILI, 2016
· Viongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
· Kamati za usimamizi wa huduma za afya Mkoa na Wilaya ya Dodoma,
· Wawakilishi wa Taasisi zisizo za Kiserikali,
· Wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya malaria,
· Waandishi wa Habari,
· Mabibi na Mabwana.
Ndugu Wananchi,
Nichukue fursa hii ya awali kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kupata fursa siku hii ya leo na kuweza kuzungumza nanyi kuhusiana na maadhimisho ya siku hii muhimu ya Malaria Duniani kwa mwaka huu (2016).
Kwa kipindi cha miaka 15 sasa, Siku ya Malaria Duniani imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka hapa nchini tarehe 25 ya mwezi Aprili.
Kihistoria siku hii ilianzishwa baada ya Wakuu wa nchi za Afrika kukutana huko Abuja nchini Nigeria mwaka 2000 na kutoa Azimio la kuwepo na siku maalumu ya kukumbushana na kuelimishana kuhusu madhara yatokanayo na ugonjwa wa malaria na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali katika udhibiti ugonjwa wa huu. Tangu wakati huo, siku ya malaria duniani imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka hapa nchini.
Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuwaelimisha wananchi ili watambue athari za ugonjwa wa malaria; wajue namna malaria inavyoambukizwa, na jinsi ya kujikinga. Aidha, maadhimisho haya pia hutumika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua dalili za malaria; na kuwahi mapema kituo cha kutolea huduma za afya, ili kupima na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kuanza kutumia dawa. Na iwapo mtu atathibitika kuwa na malaria, basi kutumia dawa na kuhakikisha kuwa anakamilisha matibabu ya malaria kulingana na maelekezo ya mtoa huduma.
Ndugu Wananchi,
Bado takwimu kutoka katika vituo vya kutolea huduma zinaonesha kuwa takribani wastani wa watu milioni 12 hupata ugonjwa wa malaria kila mwaka hapa nchini. Makundi yanayoathirika zaidi ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano (5) na mama wajawazito. Ikumbukwe ugonjwa huu wa malaria ni hatari kwa uhai wetu, maendeleo na ustawi wa Taifa letu, na ndiyo moja ya sababu kubwa inayochangia katika kupunguza kasi ya maendeleo ya jamii, hii ikiwa ni pamoja na kuleta vifo na madhara mengine yatokanayo na malaria. Jambo jema ni kuwa madhara haya yanaweza kupunguzwa na kutokomezwa kabisa kama tutatumia vizuri mikakati iliyothibitishwa katika kudhibiti ugonjwa wa Malaria hapa nchini.
Ndugu Wananchi,
Kutokana na utelekezaji wa mikakati ya udhibiti wa malaria hapa nchini kupitia wizara yangu, matunda yameanza kuonekana na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya malaria. Ripoti ya utafiti wa viashiria vya VVU/UKIMWI na Malaria inaonesha kuwa maambukizi ya malaria yamepungua kwa asilimia 50 kutoka asilimia 18 mwaka 2007/2008 hadi asilimia 10 mwaka 2011/2012. Pamoja na kupungua kwa maambukizi ya malaria, takwimu zinaonesha kuwa malaria bado ni tatizo katika maeneo ya vijijini ikilinganishwa na maeneo ya mijini ambapo maambukizi maeneo ya vijijini ni asilimia 10.7 na mijini ni asilimia 3.4. Kupungua kwa maambukizi ya malaria kunatupa kila sababu ya kujipongeza, na kumshukuru kila mdau aliyechangia kwa namna moja au nyingine katika jitihada hizi, ikijumuisha wadau wa maendeleo na mashirika ya kimataifa kwa kuwekeza katika mapambano dhidi ya malaria. Hata hivyo, bado tunayo kazi ya kufanya. Lengo ni kupunguza maambukizi ya malaria hadi asilimia 5. Mwaka 2016 na asilimia 1 ifikapo mwaka 2020. Hili linawezekana. Kila mmoja wetu anao wajibu wa kushiriki vita hii dhdi ya malaria.
Kipekee nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mhe. Dtk. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais mstaafu wa Awamu ya nne kwa jitihada zake nzuri za kupambana na malaria ndani na nje ya nchi na hadi kutunukiwa Tuzo iliyotukuka ya “White House Summit Award” mwezi Aprili 2016. Tuzo ni amepewa kutokana na kutambua jitihada na kutathimini mchango wake mkubwa na kubwa zaidi kwa kuwa mwanzilishi na kusimamia uanzishwaji wa muungano wa viongozi wa Afrika katika mapambano dhidi ya malaria “ African Leaders Malaria Alliance” (ALMA), muungano ambao hadi sasa una viongozi 49. Serikali ya Awamu ya 5 inampongeza sana na tunaahidi kumpa ushirikiano katika jitihada zake hizi njema.
Ndugu Wananchi,
Msisitizo mkubwa wa Wizara yangu ni kwa wananchi na wadau wote kuona umuhimu na kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya mikakati na afua zilizopo katika kuuthibiti ugonjwa huu. Iwapo mikakati hiyo itatekelezwa ipasavyo ni dhahiri kuwa maambukizi yataendelea kupungua kwa kiasi kikubwa na hatimaye kumaliza kabisa tatizo hili. Mikakati inayotekelezwa na Wizara kwa kushirikiana na wadau ni pamoja na:
1. Udhibiti wa mbu; kwa kutumia njia mbalimbali, mathalani kwa kutumia vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu; unyunyuziaji wa viuatilifu ukoko katika kuta ndani ya nyumba; kusafisha mazingira na kuua viluwiluwi vya mbu kwa kutumia viuadudu vya kibailojia hasa katika maeneo ya mijini.
2. Uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa malaria; kwa kuongeza kasi ya upimaji wa ugonjwa wa malaria kwa kutumia kipimo kinachotoa majibu kwa haraka (mRDT) au hadubini, na kutumia dawa mseto kama safu ya kwanza pale mgonjwa anapogundulika kuwa ana vimelea vya malaria; kuwapa wajawazito dawa ya kinga dhidi ya malaria kwa kutumia dawa ya Sulphadoxine Pyrimethamine (SP) kwa vipindi maalumu, na pia kuwapatia vyandarua vyenye viuatilifu wakati wa ujauzito.
Ndugu Wananchi,
Kwa sasa wananchi walio wengi wananufaika na mikakati na huduma mbalimbali za kupambana na malaria hapa nchini kama vile upatikanaji wa tiba sahihi ya malaria, vyandarua vyenye viuatilifu, upuliziaji wa viuatilifu ukoko katika kuta za nyumba katika Mikoa ya kanda ya Ziwa na matumizi ya viuadudu vya kibaiolojia katika sehemu zenye mazalia ya mbu, hasa katika maeneo ya mijini hususan Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa upande wa vyandarua vyenye viuatilifu, siku hii ya Malaria Duniani kwa mwaka huu inaadhimishwa ikiwa tunajivunia hatua nzuri iliyofikiwa ya zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu katika kaya bila malipo. Zoezi hili ambalo lilianza rasmi mwaka jana, linalenga katika kugawa vyandarua vyenye viuatilifu nchi nzima, isipokuwa kwa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, ambayo inatekeleza mpango wa ugawaji vyandarua kupitia wanafunzi shuleni unaojulikana kama School Net Program (SNP).
Hadi sasa tayari zoezi hili limeshafanyika katika mikoa 18 ya Tanzania Bara, ambapo jumla ya vyandarua zaidi ya million 20 vimegawiwa kwa wananchi kwa uwiano wa chandarua kimoja kwa matumizi ya watu wawili. Utekelezaji wa kampeni hii unafanyika kwa awamu, na Mikoa iliyobaki ambayo haijagawiwa vyandarua ni Mikoa minne tu ya Dar-es-Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga. Tayari uandikishaji wa wanakaya katika mikoa hii umefanyika ili kupata idadi kamili ya vyandarua vitakavyohitajika.
Wizara inatoa msisitizo kwa wananchi kulala ndani ya chandarua kila siku ili kujikinga na maambukizi ya malaria kwani Serikali imetumia gharama kubwa kwa ajili ya kuvinunua na kusambaza kwa kila kaya. Kuwa na chandarua ni jambo moja na kutumia chandarua ni jambo jingine. Nitoe rai na hamasa kwa wananchi kutumia chandarua ili kujikinga na malaria.
Sambamba na ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu, Serikali kupitia Wizara yangu ikishirikiana na wadau, inatekeleza mkakati wa upuliziaji viuatilifu ukoko katika kuta za ndani ya nyumba. Mkakati huu unatekelezwa katika baadhi ya wilaya za mikoa ya Kanda ya Ziwa zenye maambukizi makubwa ya malaria. Kwa mwaka huu zoezi la upuliziaji limefanyika katika Halmashauri 8 za Musoma, Butiama, Ngara, Missenyi, Kwimba, Bukoba Vijijini, Chato na Sengerema. Jumla ya kaya 459,212 zimepuliziwa viuatilifu ukoko na kukinga takribani jumla ya wakazi 2,296,260.
Ndugu Wananchi
Kwa upande wa matibabu na vipimo (vitendanishi) vya malaria, wizara yangu imeendelea kuhakikisha kuwa tiba sahihi inatolewa kwa wagonjwa wa malaria; hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa vipimo vya kutambua uwepo wa vimelea vya malaria kwa kutumia hadubini au kipimo kinachotoa majibu ya haraka (mRDTs) vinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya wakati wote. Aidha, vipimo vinafanyika kwa utaalamu, na dawa kutolewa kwa wale tu wanaothibitika kuwa na vimelea vya malaria. Kwa sasa vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya Serikali hapa nchini vinapima malaria kwa kutumia aidha hadubini au mRDTs. Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa wataalamu wanapatiwa mafunzo mbalimbali ili kuboresha utaalamu na weledi. Kwa kupitia juhudi hizi za Wizara yangu, kumekuwepo na ongezeko la upimaji kufikia asilimia 83 katika vituo hivyo; kiasi ambacho kinazidi lengo ambalo Wizara ilijiwekea la angalau asilimia 80.
Kwa upande wa vituo vya huduma za afya kutoka sekta binafsi, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imetoa mafunzo kwa mafundi sanifu wa maabara kutoka takribani asilimia 60 ya vituo vyote vilivyosajiliwa na Wizara kwa sasa, ambavyo vipo katika mikoa 8 ya Tanzania bara. Mikoa hiyo ni pamoja na Dar-es-Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Mbeya, Tanga, Arusha na Mwanza. Kwa Mikoa mingine iliyobaki, mafunzo yatakamilishwa katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017. Lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa huduma za upimaji zinapatikana pia katika sekta binafsi ambayo, kwa mujibu wa utafiti ngazi ya jamii (THMIS) wa mwaka 2011/12, sekta hii inahudumia takribani asilimia 40 ya watanzania wote. Natoa msisitizo kwa wananchi kuwa iwapo itatokea kupata dalili za homa, tuhakikishe kuwa tunawahi katika kituo cha kutolea huduma za afya, kisha tupime na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kuanza matibabu.
Ninapenda niwahakikishie wadau wa sekta binafsi wanaotoa huduma za afya kwamba, Wizara yangu inaendelea na jukumu la kuwawezesha watoa huduma wote ili watoe huduma ya afya kwa mujibu wa Kanuni, miongozo na taratibu zilizowekwa na Wizara. Ikumbukwe kwamba sera ya afya ni moja; na mwongozo wa matibabu na upimaji wa malaria ni mmoja.
Sambamba na vipimo, wizara yangu pia inahakikisha kuwa dawa zenye usalama, ubora na ufanisi za kutibu malaria zinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini (serikali na binafsi). Kwa upande wa vituo vya serikali pamekuwepo na ongezeko la upatikanaji wa dawa za kutibu malaria na kuwafikia wananchi kwa urahisi. Upungufu wa dawa za malaria uliokuwepo umepungua kwa kiasi kikubwa katika vituo kutoka asilimia 25 iliyokuwepo mwaka 2012 hadi asilimia 6 tu hivi sasa.
Serikali pia inashirikiana na wadau katika mpango wa utoaji wa dawa mseto za malaria kwa bei ya punguzo kupitia sekta binafsi kwa kujumuisha vituo vya kutolea huduma za afya vya binafsi na maduka ya dawa. Hii inalenga kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi atakayekosa dawa za malaria pale anapougua. Kupitia mpango huu unaojulikana kama Co-Payment Mechanism, ambao unatekelezwa nchi nzima, wananchi wanaweza kununua dawa za malaria kwa bei nafuu kabisa, toka maduka ya dawa binafsi.
Tukumbuke kuwa mazoea ya kutumia dawa bila kupima yamepitwa na wakati; kwani si kila homa ni malaria. Utafiti uliofanywa mwaka 2012 wa kutambua sababu za homa hapa nchini kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10, unaonesha wazi kuwa asilimia 62 ya watoto waligundulika kuwa na homa, homa hizo zilisababishwa na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa, wakati waliokutwa na malaria walikuwa ni asilimia 10.5 tu. Hii inaendelea kuthibitisha kuwa sio kila homa ni malaria.
Hivyo basi, tunasisitiza na kuhimiza wananchi kupima na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kuanza kutumia dawa. Na pale watakapogundulika kuwa wana malaria, basi wahakikishe wanatumia dawa na kumaliza kozi nzima ya dawa, kulingana na maelekezo ya mtoa huduma.
Ndugu Wananchi,
Ni muhimu pia kwa wanajamii kushiriki kikamilifu katika kuharibu mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji, kusafisha mifereji na kuweka mazingira safi ili kuondoa maji yaliyotuama, na hivyo kuchangia katika kupunguza maambukizi ya malaria.
Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya kutoka nchini Cuba (LABIOFAM) imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha viuadudu (biolarvicides) ambavyo vitatumika kuua viluwiluwi vya mbu katika mazalia (madimbwi, mabwawa na sehemu nyingine zinazozalisha mbu). Kiwanda kipo katika hatua za mwisho kuanza uzalishaji wa viuadudu.
Ndugu Wananchi,
Mapambano dhidi ya malaria yanahitaji juhudi za pamoja kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wanaoshughulika na udhibiti wa Malaria. Napenda nichukue fursa hii kwa niaba ya Serikali, kutoa shukrani zangu za dhati kwa wadau wetu; Mfuko wa Dunia wa kushughulikia ugonjwa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (The Global Fund), Mfuko wa Rais wa Marekani wa kushughulikia Malaria (PMI), Shirika la Misaada la Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la UNITAID, Taasisi zisizo za Kiserikali, Sekta binafsi kupitia Mpango wa Malaria Safe, Taasisi za utafiti (NIMR na Ifakara Health Institute) nikitaja kwa uchache; na bila kuwasahau wananchi katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla kwa kuwa tayari kutumia mikakati hiyo.
Ndugu Wananchi,
Nimalizie kwa kusisitiza kwamba iwapo tutaitekeleza ipasavyo mikakati niliyoitaja hapo juu, ninaamini kuwa ugonjwa wa malaria utakuwa si tatizo tena katika jamii yetu. Tunaweza kabisa kujikinga na ugonjwa wa malaria, na pia ugonjwa wa malaria unatibika na kupona kabisa iwapo mgonjwa atawahi kupata tiba sahihi mara tu baada ya kuanza kwa dalili, na kukamilisha kozi nzima ya dawa ya malaria kulingana na maelekezo ya mtoa huduma.
Ili kuendeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana, katika jitihada za kutekeleza mikakati muhimu, tunahitaji kuongeza juhudi zaidi, kutenga rasilimali fedha zaidi kwa kushirikiana na wadau wote, ili tuweze kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria hapa nchini kwa manufaa ya jamii nzima.
Nachukua fursa hii kusisitiza yafuatayo kwa wanajamii:
· Kuzingatia kupima ili kujua uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kutumia dawa.
· Kumaliza kozi ya dawa kulingana na maelekezo ya mtoa huduma.
· Kutumia vyandarua vyenye viuatilifu kila siku wakati wa kulala.
· Kuzingatia usafi wa mazingira kuzuia mazalia ya mbu.
Kwa upande wa halmashauri zote nchini nasisitiza yafuatayo:
· Kuboresha takwimu ili kujua ukubwa wa tatizo la malaria katika Halmashauri zao.
· Kuhakikisha kwamba wanaweka bajeti kwenye mipango yao ya Halmashauri (CCHP) kwa ajili ya udhibiti wa mbu.
· Kuhakikisha miongozo ya uchunguzi na tiba ya malaria inazingatiwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya umma na vya sekta binafsi.
· Kufanya ufuatiliaji katika vituo vya kutolea huduma vya umma na vya sekta binafsi ili kuboresha huduma.
Mwisho kabisa niwakumbushe kuwa zama zimebadilika “Sio kila homa ni Malaria nenda ukapime”, na “lala kwenye chandarua kila siku” kujikinga na malaria.
Matukio mbali mbali ya picha katika maadhimisho ya siku ya malaria duniani ambapo Waziri wa Afya nchini Ummy Mwalimu wakiwemo baadhi ya waandishi wa habari wameiadhimisha siku hii kwa Kupima
Malaria kwa kutumia kipimo cha haraka(mRDT)
Kulia ni mkuu wa kitengo cha udhibiti wa mmbu waenezao malaria charles dismas kutoka mpango wa Taifa wa kudhibiti malaria. |
Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria,Dkt.Renata Mandike(kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusiana na utekelezaji wa udhibiti wa malaria nchini |
Baadhi ya wataalam wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma pamoja na waandishi wa habari wakimsikiliza waziri Ummy Mwalimu |
Waandishi wa habari wakiwa wamejipanga mstari tayari kwa kupima malaria |
Mwandishi wa habari kutoka clouds media Kijah Yunus akipima malaria |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni