Alhamisi, 14 Aprili 2016

Wizara ya Afya nchini yazindua Baraza la Wataalam wa Afya ya Mazingira nchini awamu ya tatu ili kukabiliana na kuboresha huduma za afya nchini


Waziri  afya ,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto Ummy Mwalimu akiongea na wajumbe wa  baraza jipya  la usajili wa wataalam wa afya ya mazingira nchini(hawapo pichani) kushoto ni Mganga  Mkuu wa Serikali Prof: Bakari Mohammad
Baadhi ya wajumbe wa baraza hilo pamoja na maofisa mazingira wakifuatilia hotuba ya Mh. Waziri Ummy Mwalimu
Mwenyekiti mpya wa baraza la usajili wa wataalam wa afya ya mazingira nchini  Bartholomayo Ngaeje(katikati) akitoa neon la shukrani kwa waziri wa afya,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto(hayupo pichani) mara baada ya kuzinduliwa kwa baraza hilo,kulia ni msajili wa baraza hilo Iddy Hoyange na kulia ni njumbe wa baraza hilo toka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,hafla hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa wizara hiyo 
Waziri Ummy  Mwalimu akimkabidhi cheti cha Uongozi Mwenyekiti wa awamu ya kwanza Fabiani Magoma,ambapo baraza hilo uongozi hutumikia kwa miaka mitatu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu amesema Wizara ya afya imeamua kuanzisha kuanzisha Baraza la Usajili wa Wataalam wa Afya ya Mazingira kama chombo pekee cha kusimamia na kudhibiti utendaji wa Wataalamu wa  Afya Mazingira nchini kufuatia kuwepo kwa matukio ya ukiukwaji wa maadili katika utoaji wa huduma za afya ya mazingira nchini, ambapo matatizo ya kitaalam hutolewa maamuzi bila ya kuzingatia taratibu na misingi ya taaluma.

Waziri Ummy Mwalimu amesema  hayo wakati akisoma hotuba katika uzinduzi wa  Baraza la Wataalam wa Afya ya Mazingira nchini awamu ya tatu uliofanyika leo  ambapo alisema kua Afya ya Mazingira ni eneo muhimu na nyeti, ambalo utekelezaji wake unajikita zaidi katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza katika jamii yetu.

Katika hotuba hiyo Mh. Ummy amesema tunapaswa kuikumbusha jamii yetu kuwa kila mwananchi anapaswa kuwekeza kwenye usafi wa mazingira kwa kuanza  na kudumishaji usafi binafsi, usafi wa nyumba yake ya kuishi, usafi katika eneo lake la kazi, usafi katika vyombo vya usafiri, usafi katika sehemu za biashara, usafi katika nyumba za kulala wageni, usafi katika sehemu zinazouza vyakula, usafi na usalama wa vyakula na maji, usafi katika viwanda, migodi, mashamba, taasisi na nk. Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa kila sehemu inahitaji kuwekwa katika hali ya usafi na endelevu ili kudumisha kanuni za afya mazingira.

Aidha amesema Taaluma ya Afya ya Mazingira ni muhimili muhimu katika kupambana na magonjwa ya mlipuko na kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni ambapo Tanzania ni miongoni mwa mwanachama, lilitengeneza Kanuni za Afya za Kimataifa (The International Health Regulations) ambapo kwa mujibu wa Kanuni hizo wataalamu wa Afya Mazingira ndio wasimamizi wakuu wa Kanuni hizo na wana wajibu wa kuhakikisha kuwa wageni wote wanaoingia nchini kupitia katika mipaka yetu wanakaguliwa kwa kusudi la kuzuia magonjwa yanayoripotiwa Kimataifa. 

Hata hivyo Waziri Ummy amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli imeona umuhimu wa suala hili hususan pale ambapo sherehe za Uhuru zilipobadilishwa na kuadhimishwa nchi nzima kwa kufanya usafi wa mazingira ili kuonyesha kuwa maendeleo ya taifa lolote yanategemea afya za wananchi wake.

Akimalizia kusoma hotuba Waziri Ummy amesema kua matarajio ya Serikali ni kwamba kwa kutumia  Baraza hilo kama chombo cha Taaluma ya Afya Mazingira jamii yote ya watanzania itanufaika kwani Huduma ya afya ya jamii  hapa nchini itatolewa kwa viwango vinavyotakiwa na hivyo kuboresha maisha ya wananchi Baraza litasimamia na kudhibiti utoaji wa huduma ya afya ya mazingira kwa misingi ya haki na nk.

Hata hivyo Waziri Ummy alihitimisha hotuba yake kwa kutoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa Afya ya mazingira nchini kwa vile majukumu yao yanategemea sana ushirikiano weno.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni