WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO.
TAARIFA KWA UMMA TAMKO LA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO KULAANI TUKIO LA UKATILI WA KINGONO ALILOFANYIWA
MWANAMKE NA PICHA ZAKE KUSAMBAZWA KATIKA MITANDAO.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imesikitishwa na tukio la ubakaji na udhalilishwaji lililofanywa na wanaume
wawili dhidi ya mwanamke mmoja, ambaye alishurutishwa kuwa mtupu, kufanya ngono
bila ridhaa yake, kupigwa picha na kusambazwa katika mitandao ya kijamii hapa
nchini.
Wizara inalaani vikali kitendo hiki cha ukatili na udhalilishaji
kilichofanywa na wanaume wawili, ambao wamekamatwa na Polisi kwa kuhusishwa na
udhalilishaji huo.
Mazingira ya ukatili huo yanahuzunisha, kwani inaelezwa kuwa
wanaume hao kwa wakati mmoja walihusika kumwingilia kimwili pasipo ridhaa yake,
ilihali,wakimpiga picha za tukio zima la ubakaji huo. Kitendo hiki, ni ukatili
usio na kifani, maana kimefedhehesha utu wake binafsi na kudhalilisha familia
yake, na wanawake kwa ujumla.
Aidha, kitendo hiki kinaweza kusababisha madhara makubwa kwa mwanamke
huyu kimwili,kisaikolojia, kijamii na kihisia. Wizara inaamini kuwa, vitendo
hivi vya ubakaji na udhalilishaji havistahili kuvumiliwa hata kidogo, maana
vinaashiria kuwepo kwa matumizi ya nguvu, vitisho, kulazimishwa kuingiliwa, na
kuna uwezekano mkubwa wa mwanawake huyu kuwa katika hali ya hatari zaidi ambayo
inagusa maisha yake binafsi, jambo ambalo ni haki yake ya msingi.
Naomba ieleweke kuwa,
Wizara haitetei ukosefu wa uaminifu miongoni mwa wanandoa au watu wenye
mahusiano ya kimapenzi, bali tunasisitiza kwamba mwanawake sawa na binadamu
wengine anastahili na ana haki ya kuthamaniwa utu wake kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ikumbukwe kuwa uhuru na haki ya kufanya mapenzi ni hiari na kamwe
hayafanyiki kwa kulazimishwa. Navipongeza vyombo vya usalama kwa weledi wa kazi
yao ambavyo vimewasaka na kufanikisha kupatikana kwa watuhumiwa wa ukatili huo.
Serikali itahakikisha mkondo wa sheria unafuatwa kuhakikisha haki
inatendeka. Natoa wito kwa wananchi wote kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha
vitendo hivi vinakoma kabisa katika jamii zetu za Kitanzania. Hakika huu sio
utamaduni wetu! ni lazima tuhakikishe tunapambana kukomesha tabia za
udhalilishaji wa wanamke na watoto wa kike kwa nguvu zote.
Tujenge tabia ya kutoa taarifa kwa haraka matukio yote ya ukatili
dhidi ya wanawake yanapotokea katika jamii zetu. Aidha, natoa rai kwa mamlaka
zinazohusika na ulinzi na haki za wanawake zihakikishe zinaelimisha jamii
kubadilika na kuhakikisha wanawake wanalindwa maana hawa ni mama zetu, dada,
zetu, na binti zetu.
Pia, natoa wito kwa viongozi mbalimbali katika jamii kutofumbia
macho matukio ya udhalilishaji wa wanawake yanayo kiuka maadili ya jamii yetu.
Naomba kutoa rai kwa wawakilishi wa kisiasa, watendaji, na wadau wa haki za
watoto kutumia nafasi zetu katika kuelimisha wananchi kuondokana na tabia za
ukatili dhidi ya wanawake, hususani suala zima la udhalilishaji wa picha za
utupu kupitia mitandao ya kijamii, tabia ambayo imeibuka kwa kasi kubwa katika
siku za hivi karibuni.
Kamwe Taifa haliwezi kuhesabika kuwa limeendelea kama utu wa
mwanamke utwezwa na kudhalilishwa usoni mwa mataifa mengine duniani.
Erasto T. Ching’oro
Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto
16/5/2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni