Watuhumiwa wawili Zuberi Thabiti (30) na Iddy Adamu (32)
wanaodaiwa kushirikiana kufanikisha tukio la kumbaka na kumdhalilisha binti wa
miaka 21, mkulima (jina limehifadhiwa), mkazi wa Kata ya Dakawa, wilayani
Mvomero, mkoani Morogoro, wamekamatwa na kohojiwa na jeshi la polisi mkoani
humo.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya tukio hilo la kinyama usiku wa
Mei 4, mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Titii iliyoko Dakawa
ambapo Zuberi ambaye ni dereva, mkazi wa Mbarali Mbeya anadaiwa kumbaka binti
huyo huku Iddy ambaye ni mkulima, mkazi wa Makambako akirekodi picha za video
kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, baada ya kurekodi katika simu
yake, baadaye Iddy alizituma picha hizo kwa mtu aliyefahamika kwa jina la
Rajabu Salehe (26), mkazi wa Dakawa ambaye naye alizisambaza picha hizo katika
mitandao mbalimbali ya kijamii kwa watu mbalimbali.
Taarifa ya polisi imeeleza kuwa, chanzo cha tukio hilo ni kwamba,
binti huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Zuberi ambapo siku hiyo
mtuhumiwa alimpigia simu binti huyo na kumwambia aende katika nyumba hiyo ya
wageni. Taarifa hiyo ya polisi imezidi kueleza kuwa, baada ya kufika katika
chumba husika ndipo Iddy alipoingia kisha kumtaka binti huyo afanye
atakachomuelekeza huku akimshikia kisu ili asipige kelele na baada ya
kutekeleza ukatili huo (ubakaji), walimtaka asitoe siri hiyo vinginevyo
atauawa.
Aidha, baada ya tukio hilo kuripotiwa kituo cha Polisi Dakawa
Apliri 5, mwaka huu, polisi walianza uchunguzi mara moja ambapo walifanikiwa
kuwakamata jumla ya watuhumiwa 11 wakiwemo Zuberi na Iddy pamoja na
walioshiriki kuzisambaza picha hizo za udhalilishaji ambao ni; Rajabu Salehe
(26), Saidi Athumani (26), Musini Ngai (36), Saidi Mohamedi (24), John Peter
(24), Hassani Ramadhani (27), Ramadhani Ally (26), Lulu Peter (38) na Magreth
Njonjome (30), wote wakazi wa Dakawa ambapo kwa pamoja wamefunguliwa shitaka la
PICHA ZA UTUPU (P.O.N.O.GRAFIA) chini ya kifungu cha 14 (1) (a) cha sheria ya
makosa ya mtandao.
Taarifa hiyo ya polisi pia imeeleza kuwa jeshi hilo linaendelea
kuwatafuta watuhumiwa wengine huku jeshi hilo likitoa onyo kwa wananchi wote
kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kutoshiriki makosa ya
uhalifu wa kimtandao kwani sheria itachukua mkondo wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni