Haya ndio mambo 6 aliyo yachambua wakati akitoa hotuba katika bajeti ya Wizara ya Afya:-
1.Huduma ya wagonjwa wa Sickel cell,
2.watoto wenye vichwa vikubwa,
3.Huduma ya Damu salama,
4.Uhaba wa watumishi wa Afya,
5.Huduma ya Bima ya Afya,
6.Uendeshwaji wa Miradi ya wizara ya afya.
Hotuba
ya Ndg. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb Kigoma Mjini katika Bajeti ya Wizara ya
Afya Maendeleo ya Jamii Wanawake na Wazee
Azimio
la Abuja 15% ya Bajeti ya Afya, Tanzania yatenga 3%
Mheshimiwa
Spika, Kazi ya kwanza aliyofanya Rais John Magufuli katika siku zake za mwanzo
kabisa Ofisini ilihusu Wizara ya Afya. Alitembelea Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili na kutoa maagizo mbalimbali kuhusu Afya. Tuliona baadaye watendaji
wakuu wa Wizara wakihangaika huku na kule kutekeleza maagizo ya Rais.
Wengi tulitaraji kuwa Afya
za wananchi yetu zitakuwa kipaumbele kikubwa kabisa kwa Serikali. Hata hivyo
ukitazama Bajeti ya Wizara ya Afya yenye jumla ya Shilingi 845 Bilioni sawa na
3% ya Bajeti ya 2016/17 unakata tamaa. Serikali inaweza kusema kwamba Bajeti
imeongezeka kwa tarakimu lakini kimsingi imeongezeka kwenda chini ( in
decreasing order ) kwani mwaka 2015/16 Bajeti ya Wizara ilikuwa 2% kulinganisha
na asilimia 3% za mwaka huu. Nyongeza ya asilimia 1 ni ‘negligible’ kabisa hasa
ukizingatia kuwa thamani ya shilingi imeporomoka sana katika kipindi cha mwaka
mmoja uliopita.
Mheshimiwa
Spika, chukulia mfano wa Madawa ( essential medicines ) ambapo Serikali
imepanga kutumia tshs 251 bilioni mwaka 2016/17 kwa Bohari ya Madawa, lakini
katika fedha hizo tshs 131 bilioni za kulipa madeni ya miaka ya nyuma. Kimsingi
Bajeti ya madawa ya mwaka huu ni tshs 120 bilioni tu mwaka huu.
Serikali ilitangaza kuwa
Deni la MSD limehamishiwa Wizara ya Fedha, imekuwaje limerejeshwa Wizara ya
Afya? Napendekeza kuwa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya madawa mwaka huu
zitumike kwa madawa na deni la miaka ya zamani la MSD liende Wizara ya Fedha
kama ilivyokuwa imeamuriwa miaka 2 iliyopita.
Wananchi wetu wanaumizwa
sana na ukosefu wa madawa ya msingi.Utafiti na Huduma za sickle cell Hospitali
ya Muhimbili
Mheshimiwa Spika, kutokana
na ufinyu wa Bajeti miradi yetu mingi imekuwa ikitegemea wafadhili na hivyo
wafadhili wanapojitoa miradi hufa.
Miradi ya Wizara ya Fedha
inaposimama ina maana maafa ya watu wetu. Kwa mfano, kwa takribani miaka 10
Taasisi ya Wellcome Trust ilikuwa inafadhili utafiti na huduma za clinic ya
ugonjwa wa Sickle Cell katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Clinic hiyo
ilikuwa inaendeshwa na Daktari mwenye nishani za Kimataifa ( Royal Society
Pfizer Award ) Dkt. Julie Makani.
Wafadhili wamejitoa katika
mradi huu kutokana na maamuzi ya Serikali ya Uingereza kupunguza fedha za
misaada ya maendeleo na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imesimamisha huduma za
ugonjwa wa sickle cell. Hospitali ya Muhimbili sasa inawarudisha watoto wote
wenye sickle cell kwenda hospitali za Mikoa ambazo hazina huduma hii, hazina
clinic hizi.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
ni nchi ya Nne Duniani kwa kuzaa watoto wenye sickle cell baada ya Nigeria,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na India. Hivi sasa Tanzania ina watoto
takribani 12,000 wenye sickle cell. Tangu Serikali iliposimamisha huduma ya
sickle cell katika hospitali ya Muhimbili, mwanzoni mwa mwaka huu, watoto 3
tayari wamepoteza maisha kwa kukosa huduma.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inayojali wananchi wananchi wake haiwezi kamwe kukubali watoto
12,000 nchini wakose huduma. Serikali inapaswa kuendeleza clinic hii kwa
kutumia fedha za ndani. Kimsingi Serikali ilitamka kutenga fedha za Utafiti
sawa na 1% ya Pato la Taifa. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ipewe sehemu ya
fedha hizi ili kuendelea na huduma ya sickle cell. Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili ifanye mazungumzo na Dkt. Julie Makani ili kuona namna bora ya
kurudisha huduma hii.
Damu salama
Mheshimiwa
Spika, tatizo kama hilo lipo pia kwa hifadhi ya Damu salama. Wafadhili
wamejitoa kwenye mradi lakini Serikali haitengi fedha kwa ajili ya Damu salama
na matokeo yake wnanachi hawapati damu. Serikali itenge fedha kwa ajili ya
kununulia vitendanishi na upatikanaji wa Damu salama kwa wananchi wetu.
Kichwa Kikubwa
Mheshimiwa
Spika, hivi sasa kuna kampeni inayoendelea ya upasuaji wa watoto wa kichwa
kikubwa na mgongo wazi nchini nzima. Ubunifu uliofanywa na Dkt. Othman Kiloloma
kwa kupata msaada kutoka GSM Foundation unasaidia kwa sasa. Lakini kama
Serikali haijipangi maana yake ni kwamba mfadhili huyu akitoka na mradi
utakufa. Napendekeza Serikali itazame miradi hii muhimu ili iwe inatengewa
fedha kwenye Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa
Spika, nashauri Bajeti ya Wizara ya Afya iongezwe mpaka kufikia angalau tshs
1.2trn au 5% ya Pato la Taifa ili kuweza kukidhi mahitaji ya huduma za Afya kwa
Wananchi. Huduma za Afya maeneo ya vijijini yatiliwe mkazo zaidi kuliko mijini.
Uhaba wa watumishi wa Afya
Mheshimiwa
Spika, kuna tatizo kubwa sana la uhaba wa watumishi katika sekta ya Afya.
Zahanati nchini zina uhaba wa wateknolojia wa maabara 93%, wauguzi wa ngazi ya
cheti 65% na maafisa tabibu 52%. Vituo vya Afya vina uhaba wa wauguzi wa ngazi
ya cheti 65% na Hospitali za Wilaya zina uhaba wa wauguzi 77% na uhaba wa
madaktari 74%. Uhaba huu unatisha kiasi cha kupelekea baadhi ya wahudumu wa
afya kufanya kazi za maafisa tabibu.
Nilipotembelea kituo cha Afya
cha Dutwa Wilaya ya Bariadi nilikutana na Mama mhudumu wa Afya aliyefanya kazi
kama mfawidhi wa Zahanati kwa miaka zaidi ya 3. Kuna maeneo walinzi wa Vituo
vya Afya wanatoa huduma kama waganga.
Hali hii haiwezi kuendelea.
Ni lazima kuwapa huduma bora wananchi kwa kuhakikisha tunaajiri watumishi kwa
mujibu wa ikama.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya
Afya ina kibali ncha kuajiri watumishi wa Afya na mpaka Mwezi Mei 2016 hakuna
aliyeajiriwa na vibali vya ajira vinamaliza muda wake ifikapo mwisho wa Mwezi
Juni 2016. Kama ilivyopendekezwa kwenye Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya iongeze uzalishaji wa idadi ya wataalam
hususan matatibu, wataalam wa maabara na wauguzi. Mikoa ya pembeni na pembezoni
mwa nchi inapata shida sana ya watumishi wa Afya. Kwa mfano katika Mkoa wa
Kigoma hususani Jimbo la Kigoma Ujiji baadhi ya zanahani hazina kabisa matabibu
wala wauguzi. Serikali haitaweza kamwe kuleta maendeleo ya Viwanda bila ya
kuhuisha siha za wananchi.
Afya na Elimu ni sekta ambazo
lazima ziimarishwe ili kuwa na Uchumi wa Viwanda, vinginevyo hivyo viwanda
vitajengwa kwa ajili ya watu wengine na sio Watanzania.
Bodi
ya Kitaaluma ya Fiziotherapi
Mheshimiwa
Spika, Jambo linguine linalohusiana na Afya ninalopendekeza ni uanzishwaji wa
Bodi ya Wataalamu ya Fiziotherapi. Taaluma hii haina Bodi na hivyo usajili wa
wataalamu hawa na utoaji wa leseni za uendeshaji wa huduma yao hauna uratibu
mzuri na matokeo yake huduma zimekuwa zikitolewa na watu wasio na taaluma na
hata kupelekea mmomonyoko mkubwa wa maadili. Serikali ichukulie uzito kilio cha
siku nyingi cha Wataalamu wa Fiziotherapi kwa kuanzisha Bodi yao ya Usajili na
Leseni.
Bima ya Afya kwa wote
Mheshimiwa
Spika, mwisho kabisa ni kuhusu Bima ya Afya kwa Watanzania wote. Health care
financing katika nchi yetu bado ni changamoto kubwa sana na hivyo kusabibisha
huduma za afya kwa wananchi wengi kuwa za kubahatisha. Mfumo wa ‘healthcare
financing’ una maeneo matatu makuu – ukusanyaji wa mapato, ‘risk pooling’ na
manunuzi. Kila mwaka tunatenga fedha nyingi sana kwa ajili ya manunuzi ya
madawa na vifaa tiba jambo ambalo kama tungeweza kuwa na mfumo madhubuti wa
Bima ya Afya lisingekuwa ni tatizo kubwa sana maana nguvu za soko na usimamizi
tu wa Serikali zingeweza kufanya kazi hiyo kwa ufasaha sana. Serikali
inaongelea Universal Health Insurance lakini mpaka sasa hatujaonana hatua
madhubuti za kuelekea huko.
Mheshimiwa Spika, mfumo
wetu wa Bima ya Afya haujaratibiwa vizuri na matokeo yake kuna watu kimsingi
wanalipia bima za Afya mara 2 kutokana na kukosekana kwa uratibu. Hivi sasa kwa
mfano kuna skimu za bima ya Afya za kitaifa kama NHIF na CHF na vile vile fao
la Afya kutoka NSSF. Siku za karibuni PSPF na PPF wameanzisha Fao la Afya pia
kwa wachangiaji wao wa hiari.
Hata hivyo, Shirika la ILO
ambalo Tanzania ni mwanachama limeainisha mafao 9 kwa Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii na moja ya hilo ni Fao la Bima ya Afya. Kwa hiyo katika kila mchango wa
Mfanyakazi kwa mfano, kuna asilimia ya mchango inakwenda kwenye huduma ya Afya.
Hata hivyo, ukiachana na NSSF mifuko mingine haifanyi hivyo na matokeo yake
Wafanyakazi, hasa Wafanyakazi wa Serikali wanajikuta wanakatwa 20% kwenda
kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii na pia wanakatwa 6% kwenda Mfuko wa Bima ya
Afya.
Mheshimiwa
Spika, mapendekezo yangu ni kwamba Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii Nchini iwe
inapeleka michango ya Wanachama wao NHIF ili kuwe na Mfuko mmoja tu wa kitaifa.
Kwa hiyo, kutokana na
mahesabu ya kiakchurio ( actuarial ), % ya michango inayopaswa kuwa ya Afya
kutoka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iwe remitted NHIF na hivyo kila Mtanzania
ambaye anakuwa ni Mwanachama wa Mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii anakuwa ,moja
kwa moja ni mwanachama wa NHIF. Kwa maana hiyo SHIB ya NSSF iunganishwe na NHIF
na Wafanyakazi wa Serikali wasikatwe tena 6% kwenda NHIF bali PSPF, LAPF,PPF na
GEPF iremit sehemu ya michango ya wanachama wao kwa NHIF.A unified Health Insurance
Scheme inaweza kuwa chachu ya kuelekea Universal Health Insurance coverage.
Kigoma
na Ruangwa.
Mheshimiwa
Spika, katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya Ruangwa kuna
mradi wa majaribio ya kuwafanya wananchi wajiwekee akiba kupitia mfuko wa NSSF
na kasha kupata Bima ya Afya kama Fao. Mradi huu wa miaka mitano utawezesha
Halmashauri hizi 2 nchini kuwa na Universal Health Insurance coverage katika kipindi
cha miaka 2 inayokuja.
Wizara ya Afya ifuatilie
kwa karibu mradi huu ili iweze kuona kama kuna mafunzo katika juhudi za
kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa na Bima ya Afya. Nawasihi Wabunge wengine
wafuatilie tunachofanya Kigoma Ujiji na Ruangwa ili kuona namna bora ya
kufikisha huduma za Afya kwa Wananchi wa majimbo yetu.
Ninaamini kabisa kwamba
hata mradi wa tshs 50m kila kijiji ukitumika vizuri unaweza kuwa kichocheo
kikubwa kwa wananchi wetu kuweka akiba, kupata bima ya afya na hata kupata mikopo
kupitia vikundi vyao vya Ushirika.
Mheshimiwa
Spika, nawasilisha
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni