Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
Vyombo vya dola
kuanza kuwatia mbaroni watumishi hewa kwa kuwafuata na pingu majumbani.
Hatua hiyo inachukuliwa ikiwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya
tano ya Rais Dk. John Magufuli, kupambana na watendaji ambao wamekuwa
wakiisababishia hasara ya kulipa mamilioni ya shilingi kama mishahara
kwa watumishi hewa.
Habari zinasema, juzi mtumishi mmoja wa zamani katika Mkoa wa
Kigoma alifuatwa na polisi ambao walimtia mbaroni nyumbani kwao
Ubungo Kibangu Dar es Salaam.
Hilo lilifanyika juzi mchana na kuibua hofu kwa majirani ambao
waliliambia gazeti hili kuwa askari hao walifika nyumbani kwao na
mtumishi huyo na kumfunga pingu mikono na miguuni na kuondoka naye.
“Walikuja na kumkamata dada Mwajuma ambaye alikuwa hapa nyumbani kwa
mapumziko ya likizo… sasa wazazi wake walipohoji amefanya nini
waliambiwa kama wako tayari waende Mtwara na Sh milioni 21 ambazo
alilipwa kama mtumishi.
“Lakini pia inadaiwa awali alikuwa akitumia jina la mtu mwingine
alipokuwa Halmashauri ya Mtwara. Alilipwa fedha hizo kwa kutumia jina
hilo na hata alipopata kazi Kigoma alikuwa akiingiziwa mshahara kwa
jina hilo hadi kufikia kiasi hicho cha fedha.
“… na malipo haya ya mishahara alikuwa akilipwa tangu mwaka 2014 na kufikia kiasi hiki ambacho inadaiwa alikopa fedha benki.
“Baada ya tukio hili kwa kweli baba na mama yake wamechanganyikiwa na
kutangaza kuuza nyumba yao Sh milioni 40,” alisema mmoja wa majirani
walioshuhudia tukio hilo.
Gazeti hili lilipiga kambi jana katika eneo hilo la Mtaa wa Ubungo
Kibangu kuonana na wazazi wa ‘mfanyakazi huyo hewa’ lakini muda wote
nyumba ilikuwa kimya huku milango ikiwa imefungwa muda wote.
Ilipofika saa 9.00 alasiri mwandishi alimuona mtu mmoja akifungua
mlango na alipoulizwa walipo wenye nyumba alijibu kwa kifupi ‘hawapo
wenyewe wamekwenda Tanga’.
“Mimi mwenye ni mgeni hapa wenye nyumba hawapo wamekwenda Tanga kuna tatizo zito la familia,” alijibu na kuingia ndani.
Mkoani Ruvuma
Wakati huohuo, taarifa kutoka wilayani Nyasa mkoani Ruvuma,
zililieleza gazeti hili kuwa walimu watano wastaafu wamekwisha kukamatwa
na polisi kwa madai ya kupokea mishahara hewa.
Mbali na walimu hao, muuguzi mmoja pia alikamatwa.
Mmoja wa waliokumbwa na hali hiyo ni Marco Nyimbi ambaye ni mwalimu
mstaafu wa Shule ya Msingi Muungano huko Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Akizungumza na Mtanzania alisema alipigwa butwaa na kushangazwa na
hatua ya kukamatwa yeye na wenzake watano wakidaiwa kuwa ni watumishi
hewa.
“Mimi nilikuwa mtumishi halali wa Serikali. Nilistaafu kwa mujibu wa
sheria Aprili 22, 2014 na nililipwa mafao yangu Sh milioni 59 bila
matatizo yoyote,” alisema.
Alisema hata hivyo, Juni 12 mwaka huu, alitumiwa ujumbe kuwa
anahitajika kufika katika Ofisi ya Ofisa Upelelezi Liuli kwa ajili ya
kutoa maelezo ambayo hakuelezwa yalihusiana na nini.
“Sikukataa wito, nilikwenda siku iliyofuata katika ofisi hiyo lakini
sikujua niliitwa huko kwenda kufanya nini na niliwakuta wenzangu Fabian
Kilapilo tuliyekuwa tunafundisha naye Muungano, Ernest Ngayomba (Shule
ya Msingi Mengele), Philipo Maendaenda aliyekuwa akifundisha Shule ya
Sekondari Kihesa na mwenzetu mwingine mmoja.
“Tukiwa pale tulielezwa kuwa tumeisababishia Serikali kwa kuingiziwa
mishahara huku tukiwa si watumishi halali, kila mmoja alitajiwa kiasi
anachodaiwa kuchukua, mimi niliambiwa kwenye akaunti yangu walibaini
ziliingizwa Sh milioni 2.32.
“…kwa kweli nilishangazwa na kauli ile, niliwaeleza kuwa kamwe
siwezi kufanya hivyo hata siku moja na kwamba fedha ambazo niliingiziwa
na kuzitoa ni zile za mafao yangu.
“Lakini hawakunisikiliza na wakaniamuru nivue viatu niingie ndani,
waliniweka ‘lock-up’ na wenzangu wanne ambao wote tulikuwa tumestaafu
kazi siku nyingi,” alisema Nyimbi.
Alisema siku hiyo walilala mahabusu na kulipokucha saa moja asubuhi aliweza kutolewa kwa dhamana na ndugu zake.
“Nilipotolewa nilirudi nyumbani nikaenda kutazama benki (taarifa),
zangu ili nijiridhishe kama niliingiziwa fedha hizo lakini nilikuta
sikuwahi kuingiziwa fedha hizo, sasa sijui wao walitoa wapi taarifa
hizo lakini ukweli imenisikitisha mno,” alisema.
Naye Fabian Kilapino, aliliambia MTANZANIA kuwa aliitwa katika ofisi
hiyo kujieleza akidaiwa kuwekewa Sh milioni 4.64 katika akaunti yake.
“Nami nilikuwa mwalimu wa Muungano nilistaafu pamoja na mwenzangu.
Niliitwa pale na niliitikia wito na nilipokwenda nilikutana na wenzangu,
tulipoulizwa tulijibu kile tulichoamini ndiyo ukweli wenyewe.
“Lakini ghafla tulishangaa kuambiwa tuvue viatu na kuwekwa ndani hadi kesho yake,” alisema Kilapino.
Alisema alipotolewa siku ya pili alikwenda kutazama taarifa yake ya
benki ambako alikuta ziliingizwa Sh 829,000 ambazo hata hivyo hakujua
zilitumikaje.
“Nilipostaafu nililipwa vizuri kabisa mafao yangu Sh milioni 56.9…
ilikuwa Aprili 2014. Kwa kweli nilishangaa kukuta Sh 829,000 kwamba
ziliingizwa na kutoka huku nikiwa sina taarifa hiyo,” alisema.
Kilapino alisema kutokana na hali hiyo alikubali kulipa kiasi hicho
cha fedha ingawa hadi leo hajui nini kilitokea hadi zikaingizwa katika
akaunti yake.
“Sielewi hadi leo (jana) ilikuwaje fedha hizi ziliingizwa na kutolewa huku mwenyewe nikiwa sina taarifa.
“Nimekubali kuzilipa hizo fedha lakini kwa kweli tumedhalilishwa kwa
sababu walitukamata bila kufuata utaratibu wa ofisi kwani sisi tulikuwa
tunasimamiwa na Mkurugenzi hivyo tunaona hii ni sawa na uhuni,”
alisema.
MTANZANIA ilimpotafufa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angella Kairuki, kupata taarifa
kuhusiana na staili hiyo mpya ya kamatakamata ya watumishi hew,a
hakupatikana bungeni na simu yake ilikuwa imezimwa wakati wote hadi
tunakwenda mtamboni usiku.
Hivi karibuni akizungumza Dar es Salaam, Waziri Kairuki alisema
serikali imewaondoa watumishi 12,246 kwenye mfumo wa malipo ya
mishahara kwa sababu mbalimbali ikiwamo umri wa kustaafu kwa lazima,
kufukuzwa kazi, vifo na kumalizika mikataba.
Waziri Kairuki alisema kuondolewa kwa watumishi hao kumeokoa Sh bilioni 25 ambazo zingelipwa kwa watumishi hao.
Alisema fedha hizo zingepotea endapo watumishi wasingeondolewa kwenye
mfumo ikilinganishwa na watumishi 10, 295 walioondolewa kwenye mfumo
kuanzia Machi 15 hadi Aprili 30 mwaka huu.
Alisema pia kuwa watumishi hewa 1,951 wameongezeka ikiwa ni pamoja na Sh bilioni 1.8.
Waziri alisema ofisi hiyo ilitoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, wakuu
wa taasisi za umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwasilisha taarifa
ya watumishi hewa ifikapo Juni 10, mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni