Jumatatu, 11 Julai 2016

Katavi yaongoza kwa mimba za Utotoni nchini Tanzania, Waziri Ummy asema lazima tatizo hilo litafutiwe ufumbuzi!!

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema mkoa wa Katavi ndio unao ongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wasichana wanaopata mimba wakiwa na umri mdogo.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani, Mkurugenzi wa NBS Albina Chuwa amesema takwimu zinaonesha mkoa huo unaongoza kwa asilimia 36.8, Tabora 36.5, Simiyu 32.1 huku Dar es salaam ikiwa ya mwisho kwa asilimia 12.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la watu duniani (UNFPA), Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu zinazoongoza kwa tatizo hilo barani Afrika.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu ametaka jamii kutoendeleza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto wa kike na kwamba ni lazima hatua za haraka za kukabiliana na tatizo hilo zifanywe.

Naye Mkurugenzi wa huduma za afya wa Shirika la Maria Stopes,
 Dr. Joseph Komwihangiro alisema ili kupambana na hali hiyo ni lazima wasichana wapewe elimu kuhusu masuala ya uzazi ili waweze kujilinda na ndoa
za utotoni.

Takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 10 ya wasichana walio na umri mdogo wameanza kutumia njia za uzazi wa mpango.


Mkoa wa Katavi ni moja ya Mikoa mipya iliyotangazwa mwaka 2012 huku Mkoa huo ukiwa na Wilaya mbili, Wilaya ya Mlele na Mpanda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni