Jumamosi, 30 Julai 2016

Mwili wa marehemu Joseph Senga mwandishi shujaa aliepiga picha tukio la mauaji ya Mwangosi, utawasili leo saa 7:00 mchana

Marehemu Joseph Senga enzi za uhai wake

Huyu ndie Joseph Senga enzi za uhai wake, shujaa aliyehatarisha maisha yake, akasimama bila woga, akapiga picha akiwa katikati ya msitu wa askari polisi wenye silaha, huku anga ikiwa imegubikwa na moshi wa mabomu ya machozi, milio ya risasi ikisikika na kuzitunza, zikasaidia kufichua mauaji ya Mwangosi,

HISTORIA YA MAREHEMU

Jina lake halisi ni Joseph Emilio Senga. Alizaliwa Mei 22, 1957 katika wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Senga ambaye ni mtoto wa pili wa Mzee Emilio Senga ameacha watoto sita hadi kufariki kwake na mke mmoja Fridah Mockray aliyemwoa Desemba 1, 2012 katika ibada ya ndoa iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki la Sinza jijini Dar es salaam.

Alipata elimu yake ya msingi darasa la kwanza mpaka la nne katika shule ya Shushu na darasa la tano (middle school) mpaka la saba katika shule ya Ibondi na kufanikiwa kuendelea na elimu ya sekondari katika shule ya Lake, jijini Mwanza.

Senga alianza kazi rasmi ya kupiga picha mwaka 1985 akiwa na kampuni iliyokuwa ikichapisha gazeti la Uhuru, Mzalendo na Mfanyakazi ambako alidumu kwa miaka hadi mwaka 2004 wakati Tanzania Daima linaanzishwa. Mkongwe huyo ameshinda tuzo mbili za upigaji picha. 

Mpiga Picha Mkuu wa gazeti la Tanzania Daima, Joseph Senga amefariki dunia Julai 27 mwaka huu nchini India alikokwenda kwa ajili ya matibabu ya moyo.



Safari ya miaka 31 ya kuhudumu katika tasnia ya habari imefika mwisho kwa mkongwe huyo aliyekuwa miongoni mwa walioshuhudia tukio la kuzingirwa, kuteswa hadi kuuawa kinyama na askari wa Jeshi la Polisi kwa Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Daudi Mwangosi katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa Septemba 2, 2012.

Senga ambaye aliibuka Mpiga Picha Bora wa mwaka 2012 katika tuzo za EJAT alifariki dunia siku ambayo askari aliyehusika na mauaji ya Daudi Mwangosi anatupwa jela kutumikia kifungo cha miaka 15.

Taarifa ya Kampuni la Freemedia Ltd ambao ni wachapishaji wa gazeti hili kwa vyombo vya habari ilisema, “Kwa niaba ya Wafanyakazi wote unasikitika kutangaza kifo cha mfanyakazi wake Joseph Emilio Senga kilichotokea jioni ya Julai 27 mwaka huu.”

Aidha taarifa hiyo iliongeza kusema, “Kifo cha Mzee Senga kimetokea nchini India ambako alikuwa akitibiwa maradhi ya moyo kwa wiki mbili sasa tangu aondoke Julai 12 mwaka huu,” na kuongeza.

“Ofisi inachukua fursa hii kutoa pole kwa wafanyakazi wote na Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu. Uongozi wa Freemedia Ltd kwa kushirikiana na familia ya marehemu tunaendelea na taratibu za kuurejesha mwili wa marehemu nchini,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa upande wao Katibu wa Chama cha Wapigapicha za Habari Tanzania (PPAT), Mroki Mroki alisema, 

“Tumezipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kaka yetu, baba yetu kwani tuliwakuta kwenye fani hii ambayo walitusaidia kwa mengi, hakika hatutamsahau Joseph Senga kwa ucheshi wake na kujituma awapo kazi, muwazi ambaye alikuwa radhi kukosoa pale anapoona makosa katika tasnia. Apumzike kwa amani.”

Msemaji wa familia Mzee Kapama alisema, “Kifo cha kijana wetu zimetushtua sana, lakini tunajua kuwa kazi ya Mungu haina makosa taratibu za kuurejesha mwili zinafanyika kuna uwezekano mkubwa wa kuupokea jijini Dar es Salaam Jumatatu ya wiki ijayo, maziko yatafanyika Kwimba, Mwanza tutaendelea kujulishana.”

Senga ambaye ni mtoto wa pili wa Mzee Emilio Senga ameacha watoto sita hadi kufariki kwake na mke mmoja Fridah Mockray aliyemwoa Desemba 1, 2012 katika ibada ya ndoa iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki la Sinza jijini Dar es salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni