Ijumaa, 22 Julai 2016

"Nitaweka utaratibu wa kumtambua askari polisi bora wa mwezi na askari aliefanya vibaya kwa mwezi" huu ni moja ya mikakati ya Kamanda wa polisi, Muliro Jumanne Muliro wa Shinyanga!!

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne Muliro
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyaga Muliro Jumanne Muliro amesema katika kukabilia na wimbi la uharifu mkoani humo anatarajia kuandaa utaratibu maalumu wa kumtambua askari polisi bora wa mwezi na askari mwenye utendaji wa chini (mbaya) kwa mwezi.

Kamanda Muliro ameyasema hayo leo wakati
akijitambulisha kwa waandishi wa habari na kuwaeleza mikakati yake ya kikazi mkoani humo baada ya kuwasili akitokea Arusha ambapo alikuwa mkuu wa Upelelezi.

Amesema katika kuboresha mfumo wa utendaji kazi mkoani humo ataanzisha baraza la askari ambapo kutakuwa na mfumo wa kuchambuzi katika usimamizi wa idara mbalimbali, lakini pia atawatumia raia na waandishi wa habari ili kumtambua (kumpata) polisi bora wa mwezi kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya juu kisha atapewa zawadi mbele ya wenzake sanjari na kumuweka bayana askari polisi aliyefanya kazi kwa kiwango cha chini kwa mwezi na zoezi hilo litaendeshwa hadharani kupitia bwalo la polisi.

Amesma zoezi la  kumtambua polisi bora litafanywa kama njia ya kutoa motisha ya utendaji wa kazi, kupeana maonyo, jambo ambalo litasaidia kujenga taswira nzuri ya polisi mbele ya jamii.

Hata hivyo katika kufanikisha zoezi hilo amesema atafanya kazi kwa kuangalia mfumo, wa kuangalia uwezo wa kazi za kila siku kwa askari wote, kwa wiki, mwezi hadi miezi sita hadi mwaka,

“askari atambue kuwa majukumu makubwa ni kuzuia uharifu hivyo askari anapaswa atambue kwa siku amefanya nini katika kuzuia uhalifu na tusipofanya hivyo tutajikuta tumeingia katika wimbi la uhalifu ambalo hatulitarajii”, “ni muhimu kuzuia uharifu badala ya kuanza kukimbizana na matukio baada ya uhalifu kutendeka”.

Muliro amewaambia waandishi wa habari kuwa ameshafanya kikao na askari wa vitengo mbalimbali na kuwapa maelekezo ya namna atakavyo fanya nao kazi, ambapo amewataka askari polisi kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma, misingi ya kisheria na kanununi za jeshi, kutoshiriki vitendo vya rushwa, kutenda haki na kusisitiza suala la nidhamu.

Akifafanua zaidi Muliro amesema kuwa msingi mkuu wa taasisi za kijeshi duniani kote ni nidhamu na nidhamu hiyo inapaswa kuonekana moja kwa moja pia askari ni lazima aonekane ni askari kwa matendo yake, utendaji kazi wake kwa majukumu aliyokabidhiwa, maongezi, tabia akiwa ndani au nje ya ofisi pamoja na lugha yaani lugha isiyo ya kunyanyasa.

Aliongeza kuwa katika mkoa huo lipo tatizo la waganga wa kienyeji kutumia nafasi zao kupiga ramri chonganishi hali ambayo hupelekea migogoro mikubwa katika jamii licha ya kuwepo polisi katika mkoa huo, hivyo kuna haja ya kuweka mikakati ya kuzuia uhalifu kisayansi, na kwamba jamii inapaswa kueleimishwa kuhusu umuhimu wa uwepo wa wazee vikongwe na ni wajibu wa kila mwana jamii kuwapenda, kuwathamini na kuona ni bahati kuwa na wazee kama hao katika jamii.


Kamanda Muliro alihitimisha kwa kuwataka waandishi wa habari nchini kujenga tabia ya kusaidia kurekebisha kwa kueleza mazuri na mabaya badala ya kulalamika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni