Imeelezwa kuwa changamoto kubwa inayokwamisha shughuli za
kitalii katika Hifadhi ya taifa ya Ruaha na kupelekea serikali kukosa
mapato ni ubovu wa miundo mbinu.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha bw.
Moranda B. Moranda wakati akizungumza na wanahabari wanawake ambao
waliitembelea hifadhi hiyo ili kujifunza , kutalii na kujionea shughuli za
kitalii zinavyoendeshwa katika hifadhi hiyo.
Moranda amesema licha ya hifadhi hiyo kuwa kubwa kuliko zote
nchini sanjari na uwepo wa vivutio aina mbali mbali ambavyo vingeweza kuingizia
serikali mapato kutoka kwa watalii wa ndani na nje lakini serikali imeshindwa
kutupia jicho katika hifadhi hiyo .
Amesema hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba
45,000, hupokea watalii kutoka ndani na nje ya nchi kwa wastani wa 23,000 kwa
mwaka, huku baadhi ya watalii wakilazimika kukatiza ziara yao ya kutalii katika
hifadhi hiyo kutokana na kushindwa kuhimili kuifikia hifadhi hiyo kutokana na
ubovu wa miundo mbinu,
Moranda amesema ili kuifikia hifadhi hiyo wageni (watalii) hulazimika
kutumia usafiri wa barabara au anga, na kwamba usafiri wa barabara ungewezesha
watalii wengi kutoka ndani na nje ya nchi kuifikia hifadhi hiyo kwa kuwa hata
ghalama zake ni nafuu lakini kutokana na ubovu wa miundo mbinu watalii wengi
wanashindwa kufika katika hifadhi hiyo kwa kuwa wengi wao hawamudu ghalama za
usafiri wa anga kutokana na ghalama zake
kuwa juu ambapo mtalii analazimika kulipa dola
4000 kwa safari moja tu, na kwamba watalii wengi wa nje hutoka katika
bara la Ulaya na Marekani huku wengi wao wakiwa ni watu wazima ambao wamewekeza
pesa zao kwa muda mrefu tofauti na vijana ambao changamoto ya kiuchumi
inaonekana kuwa ni kubwa.
Kuhusu aina za vivutio vilivyopo katika Hifadhi hiyo Moranda
amesema licha ya kuwa na vivutio vingi ambavyo hupatikana katika hifadhi
nyingine zilizopo nchini, Hifadhi ya Taifa Ruaha ni hifadhi ya kipekee kwani
ina aina kumi (10) za simba ambao hupatikana duniani kote na ni nadra sana
kuwaona katika eneo moja, kuna wanyama aina ya Tandala wakubwa na wadogo ambao
unaweza kuwaona kwa wakati mmoja kitu ambacho ni adimu sana, kuna ndege aina
tofauti 570, mbuni ambao hupatikana kwa
wingi na kwamba kupitia mto ruaha ni rahisi kuwaona wanyama wengi kwa wakati
mmoja kwa kuwa wanyama wengi hutumia mto huo kwa ajili ya kunywa maji na jambo lingine la kipekee ni utalii wa kiutamaduni pamoja na maeneo ya
shughuli za kitamaduni kama matambiko.
Hata hivyo akazungumzia changamoto nyingine kubwa
inayoikabili hifadhi hiyo kuwa ni kukauka kwa maji katika mto Ruaha, Moranda
amesema changamoto hiyo ni kubwa na inahatarisha uhai na usalama wa wanyama
kwani wanyama wengi wanakuwa hatarini kupata magonjwa kutokana na kunywa maji
yaliyo tuama pia viumbe kama samaki nao wanakuwa hatarini kwani baadhi ya
samaki huzimia na wengine kufa kutokana na kukosa hewa hususani pale mnyama
aina ya kiboko anapojisaidia ndani ya maji kisha maji hayo yakaendelea kutuama na kuongeza kuwa changamoto nyingine ni ujangili wa kuua tembo, ujangili wa kuvua
samaki, pamoja ujangili wa kuwinda ndani ya hifadhi.
Katika kukabiliana na changamoto mbali mbali kama kukauka
kwa maji mto Ruaha na ujangili, hifadhi hiyo ilianzisha miradi mbalimbali kama,
mradi wa kuimarisha masuala ya mazingira hususani katika maeneo ambayo
yamepitiwa na bonde la ufa kama Makete, Mbarali, Wanging’ombe, Mufindi na
Kilolo, mradi huo ambao kwa sasa unaingia msimu wa pili tangu kuanzishwa kwake unaojulikana
kama “TUZO YA TANAPA YA KUHIFADHI MAZINGIRA” na kwamba katika maeneo yote hayo
kuna kuwa na mshindi 1,2 na 3 ambao mshindi wa kwanza hadi wa tatu hupewa kiasi cha fedha, na
kufafanua kuwa sababu iliyopelekea kuanzishwa kwa mradi huo ni baada ya
kugundua kuwa licha ya sababu za kisanyansi zinazopelekea maji kukauka katika
mto Ruaha lakini pia shughuli za kibinadamu zinazo fanyika katika vyanzo vya
maji vilivyopo katika bonge la ufa ni chanzo cha maji kukauka.
Pia Hifadhi hiyo ilianzisha mradi wa Ujirani mwema mwaka
1994, ili kudhibiti vitendo vya ujangili pamoja na kukabiliana na migogoro
baina hifadhi na vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo na kwamba hadi sasa zaidi
ya bilioni mbili (2) zimetumika ili kusaidia jamii katika sekta ya Afya, Elimu,
Maji na matumizi bora ya ardhi, sanjari na miradi hiyo pia kuna miradi kama kikosi
cha kufuatilia matukio kwa haraka, mradi wa mbwa wanaosaidia kufanya upekuzi wa
nyara kwa haraka na muda mfupi, mradi wa kutumia wasiri,mradi wa operation
tokomeza ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na vitendo vya kijangili
pia hifadhi hiyo imeweka namba maalumu ambayo kila mwananchi anaruhusiwa kupiga
bure muda wowote ili kutoa taarifa kwa haraka.
Moranda alimaliza kwa kuitaka serikali itupie
jicho katika suala la miundo ili kuliongezea taifa pato kupitia watalii pia
aliwapongeza wananchi Mkoani Iringa na maeneo jirani kwa kuwa na uelewa kuhusu uhifadhi ambapo
alimtaka kila mtanzania atambue kuwa ni jukumu lake kuzilinda mali asili
zilizopo nchini kwa kuwa ndio urithi wa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni