Alhamisi, 18 Mei 2017

Wakulima mkoani Mbeya wasema Kilimo Hifadhi kimeboresha afya zao!!

Wakulima wakimsikiliza kwa umakini mgani kazi ndugu  Lazaro Sukwa.

Wakulima kutoka katika wilaya za Kyela, Mbarali na Mbeya vijijini wakiwa katika moja ya shamba darasa kwa ajili ya kujifunza zaidi.
Wakulima mkoani Mbeya wamesema kilimo hifadhi kimewasaidia katika kuboresha afya zao na familia  pamoja na kuwaongezea kipato.

Wakulima hao kutoka katika wilaya za Kyela, Mbarali na Mbeya vijijini wamebainisha hayo wakati wakizungumza na mtaalamu wa Kilimo kutoka katika taasisi ya Mtandaao wa Kilimo Hifadhi Barani Afrika  ndugu Hamis Dulla Mzoba ambae alitembelea mashamba darasa yaliyopo katika kijiji cha Inyara kata ya Iyawaya na kujionea jinsi ambavyo elimu ya Kilimo Hifadhi imewakomboa wakulima kiuchuni  kiafya na kijamii

Joyce Nkamu, makamo mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima Iyawaya na Lazaro Sukwa ambae ni mgani kazi, wanasema kilimo  hifadhi ni kilimo chenye tija na kwamba ni msaada mkubwa kwa wakulima hao kwani kwa sasa wakulima hutumia gharama kidogo , muda mchache na nguvu kazi ndogo kuanzia hatua ya kuandaa mashamba hadi kufikia hatua ya kuvuna huku wakijipatia kipato kikubwa.

Hata hivyo wanaongeza kuwa kilimo hifadhi kimebadili mfumo wa maisha ya wakulima wengi ambapo awali kutokana na kilimo cha mazoeya wakulima wengi hawakuweza kujikita na shughuli zingine kama ufugaji, biashara, uvuvi nk kutokana na kutumia muda mwingi kwa shughuli za kilimo huku kipato kikiwa hakikidhi mahitaji na afya zao zikizorota kwa kutumia nguvu kazi nyingi.

Kwa upande wake muwakilishi kutoka katika taasisi ya Kilimo Hifadhi Barani Africa (ACTN) Ndg. Hamis Mzoba,  akawataka wakulima kujifunza zaidi kuhusu kanuni za kilimo na matumizi sahihi ya pembejeo ili kupata matokeo chanya ya Kilimo Hifadhi na kuleta mapinduzi ya kijani.

“Mimi ninacho washauri tuendelee kuonesha hayo matokeo chanya ambayo tumeyaona hata leo ili kuwafanya watu wengi waweze kujua na kuona faida za kilimo hifadhi ambacho kina tija, lakini pia ni vema tukafahamu kuwa kilimo hifadhi peke yake kama haujatekeleza mbinu nyingine za kilimo haitoshi kilimo hifadhi kinaendana vizuri sana na matumizi bora ya pembejeo za kilimo kama mbegu, mbolea na viuwatilifu.”

Hata hivyo akawataka wakulima kutosita ama kuto ona aibu kujifunza kwa kuwauliza  wenzao ambao wamepata matokeo chanya badala ya kuiga pasipo kujifunza kutoka kwa wakulima wenzao ambao wamepata matokeo mazuri katika kilimo kwani kwa kufanya hivyo ni hatari.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni