NA: EVELYN MKOKOI
Kufuatia ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina, iliyofanyika Jijini Dar es Salam leo
katika Manispaa ya ilala, ilohusisha ukaguzi wa Dampo la Pugu Kinyamwezi,
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kupitia Mkaguzi wa
Mazingira wa kanda ya Mashariki Bw. Jaffari Chimgege, limeitoza faini
Manispaa ya jiji ya Dar es Salaam kiasi
cha shilingi Milioni 25, kwa kosa la uchafuzi wa Mazingira wa kutohudumia Dampo
hilo ipasavyo na kupelekea harufu mbaya, vumbi na maji yenye sumu kali na kuhatarisha afya ya wakazi wa maeneo jirani
viumbe hai na mzingira kwa ujumla.
Kufuatia malalamiko ya wakazi wa mtaa wa Viwege uliyopo
katika kata ya Majoe yaliyowasilishwa na mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Bi
Amina Rashid yaliyoeleza kuwa na changamoto mbali mbali katika dampo hilo
zikiwemo za vumbi na maji yenye kemikali kwenda katika maeneo ya makazi, Naibu
Waziri Mpina, ameitaka Halmashauri ya jiji kuja na mpango mkakati utakaoweza
kuupunguzia mzigo dampo la Pugu ambalo kwa sasa linatumika kupokea takataka
zote za Halmashauri za jiji la Dar es Salaam na kuonekana kulemewa na mpango
huo uwezeshe kila manispaa kuwa na dampo lake.
Aidha Mpina alibaini kuwepo kwa madhaifu makubwa katika
ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kuondosha taka katika manispaa za jiji na
kuutaka uongozi wa jiji Hususan Mkurugenzi wa Jiji kufuatilia madeni hayo
kikamilifu, pamoja na kutoa deadline
ya uwasilishwaji wa fedha hizo “ni vyema ghahama za uondoshwaji wa taka
zikatokana na taka zenyewe na siyo kutoa fedha za kuhudumia taka kutoka katika
vyanzo vingine vya mapato. Alisisitiza Mpina.”
Mpina pia aliitaka manispaa ya jiji kutafuta namna bora ya kuondosha taka sumu na
kuelekeza taka zote za matairi katika jiji la Dar es Salaam zitafutiwe sehemu
tofauti na namna pekee ya kuzitekekeza.
Akionekana kuongea kwa hasira na msisitizo Naibu Waziri Mpina
alisema, “ Hakuna kitu nisichopenda katika utendaji wangu kama kuona taasisi za
serikali zikiwa za kwanza katika suala zima la uchafuzi wa mazingira, faini
hiyo jiji mtailipa ndani ya siku 14, na kuhakikisha mnarekebisha matobo yote yanayolalamikiwa kupitisha maji
na kupeleka katika makazi ya wananchi pamoja na kujenga mifereji ya maji ya
mvua, na maji ya sumu yaende katika mkondo sahihi wa maji hatarishi na bila
kusahau kuruhsu maji hayo baada ya kujiridhisha na vipimo vinavyotakiwa.
Awali akitoa taarifa ya hali ya mazingira na usimamizi wa taka katika Dampo la Pugu Kinyamwezi , Mkuu wa Idara ya
usimamizi taka wa jiji la hilo Bw. Shedrack Maximillian alimueleza Mpina kuwa
jiji linakabiliana na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja dampo kupata moto,
dampo kutokuwa la kisasa na maji yenye sumu kwenda katika makazi ya wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni